DKT. DUGANGE AZITAKA HALMASHAURI KUKAMILISHA MIRADI ILIYOANZISHWA NA WANANCHI

 



***********************

OR - TAMISEMI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange( Mb) amezitaka Halmashauri kutumia asilimia 40 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.

Ameelekeza hayo leo tarehe 08 Machi, 2023 baada ya kupokea taarifa ya ukusanyaji wa mapato wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya Arusha Mkoani Arusha.

Dkt. Dugange amezitaka Halmashauri kuhakikisha zinatenga asilimia 40 na kuzipeleka kwenye miradi itakayotatua kero za wananchi pamoja na kukamilisha miradi iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.

Amezitaka Halmashauri kuweka mikakati ya kukusanya mapato ili kuondokana na hali ya utegemezi wa fedha kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya utekelezaji wa  miradi ya maendeleo.

Kadhalika, Dkt. Dugange amezitaka Halmashauri kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri inaratibiwa na kutolewa kwenye vikundi vyenye sifa ili kuleta tija kwa wananchi.

“Uwekwe mpango kazi wa kuviwezesha vikundi vinavyonufaika na mikopo ya asilima 10 kwa kuwapa elimu na kuwaratibu ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi”

Halmahauri ya Arusha ilisimamia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 4.8, hadi kufikia mwezi Februari, imekusanywa bilioni 3.3 sawa na asilimia 68 ya malengo ya mwaka.

0/Post a Comment/Comments