Mke wa Hayati Magufuli, Mama Janeth Magufuli akiweka shada la maua kwenye Kaburi la mumewe.
Waziri wa Ulinzi,Inocent Bashungwa,akiteta jambo na aliyewahi kuwa katibu wa fedha kwenye serikali ya awamu ya tano,Doto James
Na Daniel Limbe,Chato
KANISA Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara,limetangaza rasmi kuiadhimisha kila mwaka siku ya kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania,Hayati Dk. John Pombe Magufuli.
Ikiwa imetimia miaka miwili tangu kifo cha Hayati Magufuli, leo Kanisa Katoliki jimbo la Rulenge Ngara, limetangaza rasmi kuiitambua na kuiadhimisha kila mwaka machi 17 ikiwa ni kumwombea toba kwa Mwenyezi Mungu na kutambua mchango wake mkubwa kwa kanisa na jamii kwa ujumla.
Askofu wa Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi, amesema Kanisa katoliki jimbo hilo limeipitisha rasmi siku hiyo ambayo itaanza kuadhimishwa kila mwaka na kwamba waumini wa kikatoliki wanapaswa kuitambua kwa kumwombea heri Hayati Magufuli.
Alikuwa kwenye Ibada ya misa takatifu ya kumwombea toba kwa Mungu,iliyofanyika leo kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mlimani Rubambangwe Chato,takribani mita 100 kutoka nyumbani kwao Hayati Magufuli.
"Siku hii sasa ni rasmi kuiadhimisha kila mwaka...mimi nitakuja hapa kila machi 17 hata kama nitakuta waamini wawili,hata kama nikiwa pekee yangu nitasali maana popote alipo askofu na kanisa liko hapo" amesema Niwemugizi.
Hata hivyo,Askofu Niwemugizi,ametumia fursa hiyo kumwombea Hayati Magufuli, msamaha kwa yeyote aliyemkwaza enzi za uhai wake na kwamba huenda aliwakosea baadhi ya watu kwa kuwa naye alikuwa binadamu kama wengine.
Akizungumza kwa niaba ya rais,Samia Suluhu Hassan,Waziri wa Ulinzi Inocent Bashungwa, mbali na kushukuru kwa utumishi mwema wa hayati Magufuli,amesema serikali itaendelea kuenzi mambo yote mazuri aliyotamani watanzania kuyapata.
"Ni miaka miwili imepita tangu tumempoteza aliyekuwa rais wetu wa awamu ya tano,Hayati Dk. Magufuli...ni ukweli usiopingika kuwa atakumbukwa sana na serikali na jamii kutokana na maono na alama zake za kimaendeleo alizozifanya kwa watanzania" amesema Bashungwa.
Kwa upande wake,aliyekuwa mke wa Hayati Magufuli, Mama Janeth Magufuli,amewapongeza watanzania kwa kuendelea kumwombea mema Hayati Magufuli sambamba na kilishukuru Kanisa Katoliki kwa kuendelea kumuenzi kipenzi cha watanzania.
Rais Magufuli alifariki machi 17 mwaka 2021 wakati akipatiwa matibabu ya moyo kwenye hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam, jambo lililotikisa nchi na kuzua simanzi kubwa kwa jamii.
Ni kutokana na nchi kutowahi kushuhudia kifo cha rais akiwa madarakani tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika.
Mwisho.



Post a Comment