Mkuu wa wilaya ya Chato,akitoa maelekezo ya serikali kwenye mkutano mkuu wa Chama kikuu cha ushirika Chato (CCU).
Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Chato(CCU) Berino Msigwa, akizungumza na waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha ushirika Chato(CCU) Greon Chandika,akiziungumza na waandishi wa habari.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama kikuu cha ushirika Chato,wakiendelea kupokea maelekezo kutoka kwa viongozi mbalimbali.
******************
Na Daniel Limbe,Chato
SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita,imeyaonya makampuni ya ununuzi wa pamba ambayo yamekuwa yakikopa zao hilo kutoka kwa wakulima kisha kutokomea baada ya msimu kumalizika
Hali hiyo inadaiwa kuwakatisha tamaa baadhi ya wakulima wa zao hilo licha ya kuwa ni miongoni mazao ya kimkakati kwenye wilaya hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Chato,Deusdedith Katwale, amefikia uamuzi wa kuyapiga marufuku makampuni hayo baada ya ofisi yake kupokea malalamiko mengi ya wakulima kukopwa na kuzurumiwa fedha zao.
Alikuwa kwenye mkutano mkuu wa kawaida wa Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Chato(CCU) ambapo pamoja na mambo mengine kimepitisha makisio ya kununua pamba kilo laki 5 kwenye msimu wa kilimo wa 2023/24.
"Ninaagiza kuanzia mwaka huu sitaki kuona watu wanaokuja kwenye wilaya hii kukopa pamba wakulima...kama hawana pesa taslimu wasije kuchukua pamba ya wakulima wetu...haiwezekani mkulima anahangaika na kilimo halafu wanakuja watu wachache kuwakopa na kuwazurumu...hii nimarufuku kuanzia msimu huu sitaki kusikia hilo".
Mwenyekiti wa CCU, Greon Chandika,amesema ili mkulima aweze kujikomboa na lindi la umaskini wa kipato,hana budi kujiunga kwenye ushirika kwa kuwa ndiko kwenye fursa nyingi za kumsaidia ukilinganisha na wanunuzi binafsi.
Hata hivyo,amesema Chama chake ni miongoni mwa vyama vya ushirika vilivyowalipa wakulima wote kwenye wilaya ya Chato na Biharamulo,huku akiwasisitiza wakulima kuendelea kulima kisasa na kuviimalisha vyama vya msingi (Amcos).
Kaimu Meneja wa chama cha ushirika wilaya ya Chato, Beno Msigwa,amesema katika msimu wa kilimo 2023/24 Chama hicho kinatarajia kuchukua mkopo kutoka benki ya wakulima (TADB) kiasi cha zaidi ya bilioni 1.4 ambazo zitasaidia kusimika mashine mpya za kukamua mafuta yatokanayo na mbegu za pamba ili kupunguza uhaba wa mafuta ya kula nchini.
Awali Ofisa mkaguzi wa ubora pamba wilaya ya Chato,Biharamulo na Muleba,Samwel Mdidi, amewanyooshea kidole baadhi ya viongozi wa Amcos ambapo amewasihi kuacha kujihusisha na wizi wa pembejeo za wakulima zenye ruzuku ya serikali na kwamba bodi ya pamba nchini haita waonea huruma kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya dora.
Mwisho.




Post a Comment