Mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Advela Bulimba,akiwasha moja ya pikipiki 41zilizokabidhiwa kwa maofisa ugani.Mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Kamishina msaidizi wa polisi Advela Bulimba,akimkabidhi pikipiki mmoja ya maofisa ugani.
Mwonekano wa pikipiki zilizogawiwa kwa maofisa ugani Biharamulo.
Mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Kamishina msaidizi wa polisi Advela Bulimba,akimkabidhi pikipiki mmoja ya maofisa ugani.
*********
Na Daniel Limbe,Biharamulo
KATIKA kukabiliana na uhaba wa chakula nchini,serikali wilayani Biharamulo mkoani Kagera imewapatia pikipiki 41 maofisa ugani wa vijiji na kata kwa lengo la kuwahudumia wakulima.
Hatua hiyo imedaiwa kuwa ukombozi mkubwa kwa wakulima kutokana na malalamiko ya muda mrefu ya kukosekana kwa huduma za ugani, hali iliyokuwa ikichangia kutozalisha kwa tija.
Akikabidhi pikipiki hizo Mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Kamishina msaidizi wa polisi,Advela Bulimba, amewataka maofisa ugani hao kuzitumia pikipiki hizo kwa malengo yanayokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuzitunza.
Ametumia fursa hiyo kuwataka maofisa ugani hao kutengeneza mipango kazi ya kuwafikia wakulima mashambani na kwamba atafuatilia ili kujua utendaji kazi wa kila mmoja na kwamba hata kuwa na huruma kumwajibisha yeyote atakaye shindwa kufikia malengo yaliyowekwa.
Awali akitoa ufafanuzi wa ugawaji wa pikipiki hizo, Ofisa kilimo wa wilaya hiyo,Bruno Ngawagala, amesema zaidi ya milioni 123 zimetumika kununua pikipiki hizo ili kuondoa uhaba wa usafiri kwa maofisa ugani ambao wamekuwa wakishindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu kutokana na umbari wa kuwafikia wakulima.
Kwamba pikipiki hizo ni utekelezaji wa ahadi ya wizara ya kilimo kwa maofisa ugani hao, na kwamba kupatikana kwa vitendea kazi hivyo utarahisisha utoaji wa elimu ya kilimo kwa wakulima hatua itakayosaidia kuzalisha kwa tija badala ya kupata mazao ya kijikimu.
Katika hatua nyingine, Ngawagala akagusia mahitaji ya wataalamu wa kilimo kwenye wilaya hiyo kuwa mahitaji ni 94 huku waliopo ni 44 na upungufu ukiwa ni watumishi 50.
Mbali na kuipongeza serikali kwa uamuzi huo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushau,amesema tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika, haikuwahi kutokea watumishi wa idara ya kilimo kupewa kipaumbele cha usafiri kama ilivyotokea na kwamba ni muda mwafaka kwa watumishi hao kuchapa kazi kwa bidii.
"Tunachotaka sasa ni kuona matokeo yenye tija kwa wakulima wetu...serikali imeamua kuwapeni vitendea kazi hivi ili viwe chachu kubwa ya ninyi kuwahudumia kikamilifu wakulima wetu ili wazalishe kwa ubora wa hali ya juu" amesema Rushau.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Inocent Mkandara, amewataka watumishi hao kujiepusha na udanganyifu wa matumizi ya pikipiki hizo badala yake zitumike kwa malengo ya kuwahudumia wakulima.
Mwisho.




Post a Comment