Picha ya mwanafunzi mjamzito.
Baadhi ya madiwani wakiendelea na kikao cha Baraza lao...
Mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Kamishna msaidizi wa polisi,Advela Bulimba,akitoa agizo la walimu wanaowapa mimba wanafunzi.
Na Daniel Limbe,Biharamulo
MKUU wa wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera,Kamishna msaidizi wa polisi,Advela Bulimba,amezuia utaratibu wa kuwahamisha vituo vya kazi walimu wa shule za msingi na sekondari wanaodaiwa kujihusisha kimapenzi na wanafunzi badala yake wasimamishwe kazi na kufikishwa mahakamani.
Aidha baadhi ya walimu hao wamekuwa wakituhumiwa kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari huku hatua kali zikiwa hazichukuliwi.
Kutokana na hali hiyo,Mkuu huyo wa wilaya amelazimika kumwagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Inocent Mkandara,kuhakikisha anawachukulia sheria kali baadhi ya walimu wote wanaotuhumiwa kwa vitendo hivyo.
Ametoa kauli hiyo leo,machi 7 kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, huku akiwasihi madiwani kumpa ushirikiano kwa kufichukua vitendo vyote viovu wanavyotendewa wanafunzi ili vikomeshwe haraka kabla ya madhara kuwa makubwa zaidi.
"Nimeletwa hapa na Mh. rais Samia Suluhu kwa sababu ameniamini kuwa naweza kumwakilisha vyema...na kabla ya kufika hapa nilipata taarifa za vitendo vya walimu kuwapa mimba wanafunzi...hahitaji kuona vitendo hivyo vina kwisha na wala sitokuwa na muhali na wote wanaoharibu ndoto za watoto wetu" amesema Bulimba.
Katika kile kinachoonekana ni kuanza kutekelezwa maagizo ya mkuu huyo wa wilaya, madiwani hao wameagiza kusimamishwa kazi mara moja,mwalimu wa kike wa shule ya sekondari Nyantakara(hakutajwa jina) anayetuhumiwa kuwauza wanafunzi wake kwa wanaume kisha kujipatia fedha haramu.
Kadhalika kusimamishwa huko kuendane na kuchunguzwa kwa tuhuma hizo na kwamba itakapothibitika afikishwe mahakamani kwa ajili ya kujibu kosa linalomkabili.
"Mie nadhani kwa huyu mwalimu wa kike wa Nyantakara anayewauza mabinti zetu wa shule kwa wanaume, asimamishwe kazi halafu achunguzwe ili ikithibitika afikishwe mahakamani...hatuwezi kuendelea kulea uovu wa namna hii...anatuchafua sisi na halmshauri yetu"
Kauli hiyo ya Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Mihayo Lutambi, ikaungwa mkono kwa makofi mengi ya madiwani hao wakiashiria kuchukuliwa hatua za haraka kwa mwalimu huyo.
Baada ya hoja hiyo kuchakatwa kwa kina na madiwani hao,hatimaye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushau, akatoa msimamo wa Baraza hilo kwa kumwagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kumsimamisha kazi haraka na uchunguzi ufanyike.
" Waheshimiwa hili lipo wazi na hakuna siri tulianza kupokea malalamiko kwenye shule moja,baadaye ya pili na ya tatu...kama haitoshi sasa wamehamia mpaka kwa wanafunzi wa shule za msingi...lazima tuchukue hatua stahiki" amesema Rushau.
Mwisho.



Post a Comment