Ofisa maendeleo ya jamii wilaya ya Biharamulo, Patricia Sao,akisoma risala mbele ya mgeno rasmi ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Kamishna msaidizi wa polisi,Advera Bulimba,akizungumza na wananchi wa Nyakahura.
Mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Kamishina msaidizi wa polisi,Advera Bulimba,akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali.
*****************
Na Daniel Limbe, Biharamulo
SERIKALI wilayani Biharamulo mkoani Kagera imewataka wananchi kuyatumia maadhimisho ya siku ya wanawake nchini kudhibiti vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo ili kujenga taifa lenye kizazi salama.
Mbali na watoto, vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake vimeendelea kuripotiwa maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo jambo linalotajwa kukwamisha jitihada za kundi hilo kufikia usawa wa kijinsia.
Mkuu wa wilaya ya Biharamulo,Kamishna msaidizi wa polisi,Advera Bulimba, akalazimika kutoa onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ulawiti na ubakaji sambamba na kulitaka jeshi la polisi kuchukua hatua kali kwa wote wanaohusika.
Alikuwa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kwa ngazi ya wilaya leo machi 8 kwenye kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo huku mamia ya wanawake wakijitokeza kupata ujumbe wa serikali.
"Lakini niviagize vyombo vya dola vihakikishe kwamba vinachukua hatua hatua za kisheria na kali kwa wale wote ambao watakuwa wanajihusisha na ukatili wa kijinsia na ukatili kwa watoto...pia nikuombe OCD upo hapa,Jeshi la polisi mchukue hatua kali kwa yule atakaye husika kumpa mimba mwanafunzi" amesema Bulimba.
Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Ofisa maendeleo ya jamii wilaya ya Biharamulo, Patricia Sao, ameelezea changamoto zinazowakabili wanawake wilayani humo ikiwa ni pamoja na kukosa raslimali zinazoweza kuwasaidia kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha.
"Wanawake wengi hawana raslimali zinazowawezesha kukopa kwenye taasisi za kifedha hivyo kushindwa kutumia kikamilifu fursa za kiteknolojia na kuwa wabinifu".
"Pia ndoa za utotoni,umasikini wa kipato umekuwa ukisababisha wanawake na wasichana wanaoishi katika kipato duni kuathirika na vitendo viovu na unyanyasaji wa kijinsia" amesema Sao.
Diwani wa Kata ya Nyakahura, Apornal Mugalula, amewasihi wanawake kusimama kidete kuhakikisha watoto wote wa kike wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa ili kuharakisha upatikanaji wa mabadiliko ya kiteknolojia kwa jinsia zote.
Mwisho.




Post a Comment