EMAIL: issahmohamedtz@gmail.com
Zaidi ya wakulima Milioni tatu wanatarjiwa kufikiwa ifikapo mwaka 2025 nchini katika matumizi ya bima ya mazao itakayo wawezesha kujikinga na majanga mbalimbali yanayoathiri shughuli za kilimo ikiwemo ukame, mafuriko na magonjwa ya mimea.
Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kupunguza gharama na kutoa unafuu katika bima za kilimo ili kuwawezesha wakulima kuziwekea bima shughuli za kilimo na pia kuvutia wakulima wengi kutumia huduma za bima.
Akizungumza Jijini Dar es salaam katika uzinduzi wa huduma ya bima hiyo Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Mbolea ya –YARA, Winstone Odhiambo amesema kupitia mpango wake wa Africaconnect imezindua huduma mpya ya Bima yenye lengo la kuwalinda wakulima wa Tanzania dhidi ya kuharibika kwa mazao itokanayo na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kama vile hali mbaya ya hewa.
‘’Tupo hapa leo kuzindua rasmi huduma mpya ya kuwalinda wakulima watanzania dhidi ya hasara yatokanayo na mabadilikoya TabiaNchi, kupitia mpango wa Africaconnect tutakua tukitoa bima ya mazao kupitia kampuni ya Bima ya Jubilee insurance’’ Amesema Odhiambo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa benki ya Equity Isabela Maganga amesema tayari wakulima 1400 wa mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Arusha kwa Mwaka 2022, walinufaika na mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1 kutoka benki ya Equity kupitia mpango wa Africaconnect.
‘’Tanzania inataka ijitosheleze kwa chakula na ilishe Dunia nzima hivyo ujio wa kampuni ya bima ya Jubilee itasaidia kufidia majanga ya asili wakulima wa Taifa hili’’ amesema Bi Maganga.
Deodath Mtei ambaye ni Meneja wa masuala ya Kidigitali Nchi za Tanzania na Rwanda amesema awamu ya pili ya Mpango huo utaorodhesha wakulima wa mazao ya mahindi, kahawa, viazi mbatata pamoja na alizeti.
Africaconnect ni huduma ya kidigitali iliyobuniwa mahususi kuwasaidia wakulima katika msaada wa kifedha, pembejeo bora, wataalamu wa kilimo pamoja na kukuza ustawi wa mkulima mdogo na kuongeza usalama wa chakula.
Post a Comment