Mkuu wa wilaya ya Chato,Deusdedith Katwale,akizungumza na waandishi wa habari.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wilayani Chato.
Mwenyekiti wa kamati ya amani wilaya ya Chato, Abdulrahman Ismail, akitoa dua ya kuitakia amani Tamzania baada ya kutimiza miaka 59 ya Muungano."""""""""""""
Na Daniel Limbe,Chato
SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imempongeza rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kufanya maridhiano ya kisiasa nchini, jambo linalotajwa kukuza uhuru wa kidemokrasia,amani na upendo.
Pongezi hizo zimetolewa leo wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar huku viongozi waasisi wa muungano huo wakiendelea kukumbukwa kwa uamuzi wa busara ambao umeimalisha amani na mshikamano kwa taifa.
Mkuu wa wilaya ya Chato,Deusdedith Katwale,amesema watanzania hawana budi kuwashukuru Hayati Baba wa Taifa,Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume kwa kukubali kuziunganisha nchi zao kwa maslahi mapana ya taifa na sasa matunda ya ndoto zao yanaonekana.
Mbali na viongozi hao,ametumia fursa hiyo kumpongeza rais Samia Suluhu Hassan,kwa kukubali kuketi meza moja ya maridhiano na viongozi wa vyama vya siasa nchini,na kwamba uamuzi huo unalenga kuimalisha mshikamano wa kitaifa ambao ulikusudiwa na waasisi wa taifa letu.
Amesema maadhimisho hayo yanapaswa kwenda sambamba na wananchi kuendelea kudumisha uhuru,umoja,amani,upendo na mshikamano ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kujikomboa na lindi la umaskini wa kipato.
"Niwaombe wananchi wa wilaya ya Chato kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kujikwamua na lindi la umaskini wa vipato...niwakumbushe wakulima kuendelea kuzitumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kwa kulima mazao ya muda mfupi na yanayostahimili ukame" amesema Katwale.
Mwenyekiti wa kamati ya amani kutoka viongozi wa dini wa wilaya ya Chato,ambaye pia ni Shekhe wa wilaya hiyo,Abdulrhman Ismail,ameipongeza serikali kwa kuendelea kuimalisha ulinzi na usalama wa taifa na kwamba miaka 59 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni tunu inayopaswa kuendelea kulindwa na kuenziwa.
"Sisi viongozi wa dini tunaipongeza sana serikali kwa kuendelea kuimalisha amani na mshikamano kwa wananchi wetu...pasipo kuwa na amani hata waumini wetu hawawezi kufika miskitini na makanisani...ndiyo maana tunaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha wananchi wetu wanaendelea kuitunza amani iliyopo tangu waasisi wa nchi zetu walipoamua kututengenezea nchi inayoitwa Tanzania" amesema Shekhe Ismail.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa umoja wa wazee wilaya ya Chato,Samwel Bigambo, amesema Tanzania ina kila sababu ya kusherehekea muungano ambao umedumu kwa takribani miaka 59 tangu kuanzishwa kwake, na kwamba zipo nchi ambazo zilijaribu kuungana na kisha kusambaratika ukilinganisha na nchi yetu.
"Tumetoka mbali sana ukilinganisha na hapa tulipo...wakati sisi tukiwa vijana hapakuwa na miundo mbinu mingi ya maendeleo kama ilivyo sasa, yote haya yamefanyika Zanzibar hali kadhalika huku Tanzania bara...kwa hiyo tuna kila sababu ya kumshukuru rais wetu Samia kwa kazi anazofanya kwa kuendelea kufanya maendeleo kwa nchi yetu na kuulinda Muungano kwa nguvu zote" amesema Bigambo.
Mwisho.



Post a Comment