Mwonekano wa kituo cha polisi Mganza baada ya kuvunjwa na kuchomwa moto.
Mkuu wa mkoa wa Geita,Marthine Shigella,akizungumza na wananchi wa kata ya Mganza.
**********
Na Daniel Limbe,Geita
TANZANIA ni miongoni mwa nchi chache duniani zinazosifika kwa kudumisha misingi ya amani na utulivu,jambo linalowavutia hata baadhi ya mataifa mengine kukimbilia nchini kwetu kupata hifadhi baada ya kutokea machafuko kwenye nchi zao.
Ndiyo maana siyo ajabu kusikia ikitajwa kuwa ni kisiwa cha amani na kimbilio la wasio na amani nchini mwao.
Sifa hizo siyo jambo la kubeza hata kidogo, ni kutokana na misingi bora iliyoasisiwa na viongozi wetu tangu nchi yetu alipopata uhuru wake mwaka 1961.
Pamoja na ukweli huo,zipo dalili mbaya zinazoweza kuondoa kabisa heshima ya taifa letu iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa mapema kukabiliana na matishio ya ki usalama ambayo yameanza kuota mizizi taratibu.
Matishio hayo ni pamoja na vitendo vya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mikononi na kupuuza msingi wa utawala wa sheria ambao ndiyo mwongozo wa kila raia kutii na kuufuata.
Machi 30 mwaka huu, inabaki kuwa kumbukumbu mbaya kwa masikio ya watanzania baada ya kitendo kiovu kilichofanywa na baadhi ya wananchi kuvunja na kuchoma moto kituo cha polisi Mganza kilichopo wilayani Chato mkoani Geita.
Uamuzi huo ulitokana na uvumi wa baadhi ya watu waliolituhumu jeshi la polisi kusababisha kifo cha kijana Enos Misalaba(33) aliyefariki wakati akipatiwa matibabu kituo cha afya Mganza ikiwa ni siku moja baada ya kukamatwa machi 27 na kuwekwa mahabusu ya polisi kwa tuhuma za wizi wa betri la gari.
Hata hivyo, machi 28 kijana huyo alipoteza maisha wakati akiendelea kupatiwa matibabu,jambo ambalo liliwatia hofu kubwa baadhi ya wananchi kwa madai kuwa polisi ndiyo chanzo cha kifo hicho na kuwataka wawajibike.
Mbali na ndugu wa marehemu kuridhia kuchukua mwili wa kijana wao kwaajili ya taratibu za mazishi,kiliibuka kikundi cha baadhi ya watu wakazuia kuzikwa mwili huo kwa madai ya kutoridhishwa na maelezo ya kifo hicho.
Mvutano huo ukasababisha kutwaliwa kwa nguvu mwili wa marehemu kwa lengo la kwenda kuutelekeza kwenye kituo hicho cha polisi, ikiwa ni ishara ya kukerwa na vitendo vya unyanyaswaji wa raia.
Mbali na uamuzi huo,kikundi hicho hakikukomea hapo kiliendelea kuhamasisha wananchi ambao nao pasipo kujua walijikuta wakiingia kwenye mkumbo na kuvamia kituo cha polisi hatimaye kuvunja na kuchoma moto jengo na nyaraka mbali mbali zilizokuwa ndani yake.
UCHUNGUZI WETU.
Katika uchunguzi wetu umebaini kuwa nguvu kubwa ya wananchi hao kuvamia,kuvunja na kuchoma moto kituo cha polisi inatokana na maumivu makubwa ya muda mrefu ya kukamatwa,kujeruhiwa na baadhi yao kupoteza maisha kutokana na doria zinazofanywa kwa kushitukiza ndani ya ziwa viktoria na hifadhi ya taifa ya Burigi-Chato.
Aidha machungu ya mioyo ya watu hao hayajatibiwa muda mrefu kutokana na viongozi wa serikali kutowafikia na kusikiliza kero zao ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu,badala yake wanaamini maelezo ya upande mmoja wa shilingi huku wakiwa maofsini.
Ikumbukwe kuwa wananchi wengi wanaoishi kwenye kata ya Mganza,hukidhi mahitaji yao ya kila siku kwa kujishughulisha na uvuvi wa samaki ndani ya ziwa viktoria huku baadhi yao wakifanya shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi ya taifa ya Burigi-Chato kinyume cha sheria.
Kutokana na ukweli huo, baadhi ya wavuvi huvutiwa na wingi wa samaki waliopo kwenye hifadhi ya kisiwa cha Rubondo ambapo hulazimika kuingia kinyume cha sheria na kufanya uvuvi haramu kwa lengo la kujipatia kipato kikubwa.
Hata hivyo makusudio yao hugeuka majonzi wanapokamatwa na askari wa hifadhi hiyo ambapo hupewa adhabu mbalimbali kabla ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mbali na hifadhi ya kisiwa cha rubondo, upande wa pili wa kata hiyo inapakana na hifadhi ya taifa ya Burigi -Chato, ambapo baadhi ya wananchi hufanya kazi ya ufugaji, uchomaji mkaa, kupasua mbao na wengine kukata miti ya kujengea makazi yao.
Shughuli hizo zote haziruhusiwi kufanyika ndani ya maeneo ya hifadhi za taifa kutokana na sheria taratibu na kanuni za uhifadhi nchini.
Aidha kitendo cha kukamatwa na kupelekwa mahabusu ya kituo cha polisi Mganza kabla ya kufikishwa mahakamani, wananchi hutafsiri kuwa huo ni unyanyaswaji unafanywa na polisi kwa kushirikiana na wahifadhi wa mamlaka hizo.
Mkusanyiko wa machungu ya adhabu wanazokutana nazo kutoka kwenye hifadhi za taifa pamoja na ufinyu wa elimu kwa jamii namna wanavyotakiwa kushirikiana na vyombo hivyo ni miongoni mwa sababu kuu za wananchi kuchukua uamuzi huo mbaya kwa taswira ya taifa letu.
Mmoja wa wasiri wetu ( jina tumelihifadhi) anasema kifo cha marehemu Misalaba kilitoa mwanya wa wananchi kufikisha kwa haraka ujumbe wao kwa serikali kuhusiana na maumivu ya mioyo yao yaliyodumu kwa muda mrefu pasipo kupatiwa ufumbuzi.
"Ndugu mwandishi, ukitazama kwa kina utaona kabisa kuwa kosa lile lilikuwa haliendani na adhabu iliyotolewa na wananchi...maana hakuna hata mmoja aliyeshuhudia marehemu misalaba akipigwa na polisi na amekufa akiwa kituo cha afya wala siyo mokononi mwa polisi".
"Ni kweli wapo baadhi ya polisi ambao siyo wazuri...lakini tunampongeza sana mkuu wa kituo chetu(hakumtaja jina) kwa maana hufanya kazi kubwa ya kuwadhibiti wanapokwenda kinyume maadili yao".
Anasema tatizo kubwa ni wananchi kudhibitiwa kufanya shughuli za uvuvi jirani na hifadhi ya kisiwa cha rubondo ambapo baadhi yao hukamatwa na kuingizwa kwenye eneo la hifadhi kisha kuteswa na kutakiwa kutoa fedha na ikikosekana hupelekwa kwenye kituo hicho cha polisi na wengine hupelekwa geita mjini kabla ya kufikishwa mahakamani.
Katika hatua nyingine,taarifa toka ndani ya jeshi la polisi zinaeleza kuwa uzembe wa baadhi ya viongozi wa jeshi la polisi kuchelewa kufika eneo la tukio mapema ni moja ya sababu ya askari waliokuwa zamu kuelemewa nguvu na wananchi.
Nikutokana na intelejensia kuonyesha mapema kuwepo kwa uvunjifu wa amani unaopangwa na baadhi ya wananchi kwa kisingizio cha kifo cha Misalaba.
Pia inaelezwa kuwa kituo hicho ni miongoni mwa vituo vikubwa kwenye wilaya ya Chato (IR) ambapo kinapaswa kuwa askari polisi wasiopungua 10 na kuendelea licha ya kwamba kimekuwa kikihudumiwa na askari wanne pekee.
KAULI YA MKUU WA MKOA
Mkuu wa mkoa wa Geita,Marthine Shigella,ni miongoni mwa viongozi wa Umma waliofika eneo la tukio la kujionea uharibifu huo kabla ya kuzungumza na wananchi wa Mganza.
Mbali na kuchukuzwa na kitendo hicho,aliowaonya wananchi na kuwataka kuacha kujichukulia sheria mkononi badala yake iwapo wanamalalamiko yao wanapaswa kuyafikisha kwa viongozi wa serikali ikiwemo ofisi ya mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa.
"Mie ni mkuu wa mkoa nisiye penda uongo na siyo mnafiki napenda kueleza kilichonyooka...kuweni na imani na jeshi la polisi,kuweni na imani na vyombo vya ulinzi na usalama na kuweni na imani serikali ya rais Samia Suluhu Hassan....serikali yenu ipo makini na haihitaji kunyanyasana"
"Awali niliwaambia mie siyo mnafiki, kitendo mlichokifanya wananchi wa hapa Mganza hakikubariki hata kidogo...kama mlikuwa na malalamiko yenu bado mlikuwa na nafasi kubwa sana ya kufikisha kwenye uongozi...mgefika kwa mkuu wa wilaya au mgekuja kwangu mkuu wa mkoa nikawasikiliza badala ya uamuzi mliouchukua".
Akatumia fursa hiyo kuwataka kutorudia tena kufanya uharifu kama huo kwa madai iwapo vitendo hivyo vitaendelea kushamili vitaondoa taswira nzuri ya nchi yetu ndani na hata kimataifa.
"Kwahiyo ndugu zangu nataka niwasihi sana kwamba kuchukua sheria mkononi siyo jambo jema na halikubariki...si kwa mtu mmoja mmoja,siyo kwa kituo cha polisi,siyo kwa kituo cha afya,shule,ofisi ya kijiji wala ofisi ya mwenyekiti wa kitongoji...tukijenga huo utamaduni ni hatari kwa ustawi wetu na ustawi wa taifa letu" alisema Shigella.
"Unapovamia chombo kama hiki cha polisi ujue hakikai hivi hivi...moja ya kazi ya polisi ni kujihami, jeshi la polisi lipo kwaajili ya kuwalinda ninyi...leo tungevamiwa hapa halafu jeshi la polisi likakosa silaha ya kujihami ni ninyi hawa hawa mgelilalamikia jeshi hilo...kwahiyo kitendo mlichokifanya kiwe mwanza na mwisho".
Hata hivyo,Shigella ameahidi kufanya mikutano ya hadhara na wananchi hao ili kusikiliza kero zao,huku akikiri wazi kuwa hajawahi kuzungumza na wananchi hao tangu alipoteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Geita takribani miezi sita iliyopita.
NINI KIFANYIKE
Ni wakati muafaka kwa viongozi wa umma kuzungumza na wananchi mara kwa mara ili kupokea kero na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka badala ya kusubili kutokea uvunjifu wa amani.
Wananchi waelimishwe namna bora ya kushirikiana na majeshi ya ulinzi na usalama kudumisha amani na utulivu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia raslimali za nchi kwenye hifadhi za taifa watumie nguvu za kadri kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria haraka.
Viongozi wa Umma wazitumie nafasi zao kwa kutambua kuwa wanawatumikia wananchi na kujiepusha na vitendo vya kuomba rushwa na kuwanyanyasa wasiokuwa na pesa za kuwapa ili kutoa msamaha wa makosa yaliyotendwa.
Wananchi watambue kuwa wanalo jukumu la kutii na kuheshimu mamlaka zilizowekwa kwa mujibu wa katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Wananchi wajenge utamaduni wa kueleza duku duku zao hadharani ili zifanyiwe kazi haraka badala ya kulimbikiza maumivu yanayoweza kuathiri ustawi mzuri wa taifa letu.
Pia baadhi ya askari polisi wenye kulalamikiwa kwa utendaji kazi mbovu wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye kupuuza falsafa za polisi jamii na ulinzi shirikishi.
Uchunguzi wa kina uendelee kufanywa na vyombo mbalimbali vya uchunguzi ili kuwabaini watu wote waliohusika na uvamizi wa kituo hicho pasipo kumwonea mtu kutokana na itikadi za kisiasa,kidini wala kabira kisha wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazo wakabili.
Mwisho.



Post a Comment