UJENZI HOLELA NYUMBA ZA IBADA WATAJWA KUWA KERO

 








*************

Na: Issa Mohamed –Dar es salaam.

Email: issahmohamedtz@gmail.com

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam CPA Amos Makala ameonesha kutoridhishwa na ujenzi holela wa nyumba za ibada pamoja na kumbi za starehe katika makazi ya watu hali inayozalisha kero na malalamiko ya mara kwa mara kwa Wananchi.

Ametoa kauli hiyo katika kikao cha wadau pamoja na watendaji wa serikali kilicholenga kupata maoni kuhusu udhibiti wa mifuko ya Plastiki, Kelele na mitetemo kilichoandaliwa na Baraza la Taifa la hifadhi na usimamizi wa Mazingira –NEMC kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Amesema Serikali inathamini mchango wa Taasisi za Dini lakini haitavumilia kuona baadhi ya nyumba za ibada pamoja na kumbi za starehe inageuka kuwa kero ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaelekeza watendaji wa serikali za mitaa kushirikiana na –NEMC katika kulisimamia hilo.

‘’Furaha usijipe wewe ukapeleka kero kwa watu wengine, ndomana kuna taratibu ambapo wengi wao wamekuwa wakitafuta huruma pale ambapo serikali inafungua hivyo lazima tufate sheria’’ Amesema RC CPA Makala.

Sambamba na hilo CPA Makala amesema Serikali ya Mkoa huo inatarajia kuanzisha oparesheni nyingine kwa wale wote wanaoagiza, kusambaza au kutumia mifuko ya Plastiki na yeyote atakaebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

‘’Wale ambao walifuata utaratibu viwanda vyao vimefungiwa lakini hawa wajanja wanaendelea kufanya biashara hilo haliwezekani na tutaanzisha oparesheni nyingine kabambe baada ya Semina hii’’ Amebainisha RC CPA Makala.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza laTaifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira –NEMC, Dkt Samuel Gwamaka amesema serikali kwa kushirikiana na wadau watahakikisha wanashirikiana kwa pamoja ili kutekeleza sheria ya mwaka 2014.

‘’Kuna kundi moja la nyumba za ibada hatujaliunganisha lakini tutakutana nalo kutokana na shughuli zinazofanyika ni tofauti kutokana na kupata kero nyingi licha ya baraza kujitahidi kuzitatu’’ Ameeleza Gwamaka.

Itakumbukwa kuwa Juni mosi 2019 serikali ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya Plastiki Nchini lengo ni kupunguza uchafuzi wa Mazingira pamoja na kulinda viumbe hai ikiwemo viumbe Bahari.

0/Post a Comment/Comments