Mkuu wa wilaya ya Chato,Deusdedith Katwale,akitoa pongezi kwa baadhi ya watumishi wa wilaya hiyo.
Mganga mkuu wa wilaya ya Chato,Dk. Eugen Rutaisire,akizungumza na waandishi wa habari.
Mganga mkuu wa wilaya ya Chato,Dk. Eugen Rutaisire,akizungumza na waandishi wa habari.
Baadhi ya madiwani wakichangia maoni yao ya pongezi kwa baadhi ya watumishi wa umma Chato.
Meneja wa Tarura wilaya ya Chato,Mhandisi Ernest Nyanda,akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za madiwani. *********
*Takribani dakika 15 zatumika kuwapongeza*
Na Daniel Limbe,Chato
KATIKA kile kinachoonyesha kutambua thamani ya mchango wa baadhi ya watumishi wa umma kwenye wilaya ya Chato mkoani Geita, takribabi dakika 15 zimetumika kumpongeza mganga mkuu wa wilaya hiyo pamoja na meneja wa wakala wa barabara za mjini na vijijini(Tarura).
Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chato,huku mkuu wa wilaya hiyo,Deusdedith Katwale,akishindwa kuficha hisia zake na kumwaga pongezi nyingi kwa watumishi hao.
"Naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana mganga mkuu wa hospitali ya wilaya yetu...huyu mtumishi tangu amekuja Chato amekuwa na ushirikiano mkubwa sana kwangu na kwa wananchi...popote panapotokea changamoto za huduma za afya anakwenda haraka na kutatua kwa wakati"
"Kila napomhitaji anafika na haijalishi ni mchana ama usiku, tena hasubiri kutumia gari la serikali...anatumia gari lake mwenyewe kwenda kutatua changamoto za wananchi wetu...nikuombe uendelee na moyo huo na ninaamini mwenyezi Mungu ndiye atakaye kulipa sawasawa na matendo yako mema" amesema Katwale.
Kadhalika ametoa pongezi kwa Meneja wa wakala wa barabara za mjini na vijijini (Tarura) kutokana na utendaji wake uliotukuka na kwamba amekuwa msaada mkubwa kwa jamii kutokana na utatuzi wa changamoto za barabara ambazo zipo nje ya bajeti yake.
"Mtumishi huyu naye anahitaji pongezi nyingi kutokana na kufanya kazi kwa kujituma na kwa moyo wa uzalendo...mara kadhaa nimekuwa namwomba kutusaidia baadhi ya maeneo korofi anakubali na kwenda kutatua licha ya kuwa maeneo hayo hayana bajeti ya fedha kutoka Tarura"amesema Katwale.
Mbali na mkuu huyo wa wilaya, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Christian Manunga,naye ametumia fursa hiyo kuwaelezea watumishi hao sambamba na kuwapongeza kwa mchango wa kizalendo katika kuitumikia jamii.
Hali kadhalika,amewataka watumishi wengine wa umma kuiga mfano wa watumishi hao ili kuongeza imani ya wananchi kupata huduma bora na za viwango vya hali ya juu kutoka kwa watumishi walioaminiwa na serikali.
Mganga mkuu wa wilaya hiyo,Dk. Eugen Rutaisire, amesema siri ya mafanikio hayo imetokana na kuhuisha mfumo wa mahusiano mazuri na watumishi wengine waliopo chini yake sambamba kutatua changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake,Meneja wa Tarura wilaya ya Chato, Mhandisi Ernest Nyanda, amewashukuru viongozi mbalimbali kutambua mchango wake na taasisi yake kwa ujumla huku akiahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa zaidi ili kuhakikisha wanapunguza changamoto zinazowakabili wananchi.
Mwisho.




Post a Comment