.....................
Mkuu wa mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego amesema Mkoa wake umejipanga vema kuanza msimu wa kilimo wa mwaka 2023/ 2024 hususan katika eneo la upatikanaji na usambazaji wa mbolea kwa wakulima kwa wakati.
Mhe. Dendego ameyasema hayo mwishoni mwa wiki ofisini kwake alipotembelewa na ujumbe
kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka Dkt. Stephan Ngailo.
Dendego amesema kuwa mikakati mbalimbali inaandaliwa na mkoa kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbolea kwa
wakati ikiwemo kuwaelimisha wakulima wanunue mbolea mapema wakati wanapovuna na kuuza mazao yao kuliko kusubiri wakati wa kupanda.
Amesena mkoa wake pia unawahamasisha wakulima waanze kujisajili mapema ili waweze kunufaika na mpango wa mbolea za ruzuku awamu ya pili uliotolewa na serikali.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Dendego amesema katika msimu wa 2022/2023 mkoa wake ulinufaika na tani 32,000 za mbolea ambazo ni sawa na asilimia 72
Akizungumza awali katika kikao hicho, Dkt. Stephan Ngailo alisema ili kutatua changamoto za usambazaji wa mbolea zilizojitokeza msimu uliopita, Mamlaka imejipanga kuongeza vituo vya usambazaji karibu na wakulima.
Dkt. Ngailo ameuomba uongozi wa Mkoa kuainisha maghala ya serikali yaliyopo kwenye Halmashauri zao ili yatumike kuhifadhia na kuuzia mbolea kwa wakulima.
Aidha katika msimu ujao, Dkt. Ngailo ameomba vyama vya ushirika vitumike kama vituo vya mauzo ili kupanua mtandao wa usambazaji wa mbolea.

Post a Comment