Diwani wa Kata ya Chato,Mange Ludomya, akitoa hoja ndani ya kikao.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chato,Christian Manunga,akiongea na madiwani wa halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa kamati ya Elimu,Afya na Maji,Josephat Manyenye,akitoa majibu ya hoja zilizoibuliwa na madiwani **********
Na Daniel Limbe,Chato
HALMASHAURI ya wilaya ya Chato mkoani Geita,inatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni 30 kukamilisha ujenzi wa uzio wa shule ya msingi aliyosoma aliyekuwa rais wa Tanzania,Hayati Dk. John Magufuli, baada ya ujenzi huo kusimama kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Ujenzi huo ulianza kwa jitihada za aliyekuwa mkuu wa mkoa huo,Robert Gabriel, ambaye alisimamia utekelezaji huo na baada ya kifo cha Hayati magufuli ujenzi ulisimama pasipo kukamilika huku jamii ikiwa haijui hatma yake.
Kutokana na hali hiyo,Diwani wa kata ya Chato,Mange Ludomya,akalazimika kuhoji ndani ya kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo,akitaka kujua mpango wa serikali kukamilisha ujenzi huo ili kunusuru maisha ya watoto wanaosoma kwenye shule hiyo ikiwa ni sambamba na kuinua taaluma za wanafunzi.
Mbali na mwenyekiti wa kamati ya Elimu,Afya na Maji,Josephat Manyenye,kukiri ujenzi huo kusimama kutokana na sababu mbalimbali,amesema ipo haja kubwa ya kuheshimu ahadi za viongozi wa Umma ikiwemo ahadi ya aliyekuwa mkuu wa mkoa huo kabla ya kuhamishwa mkoani humo na ujenzi kusimama.
Hata hivyo,Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Christian Manunga,amesema serikali kuu tayali imeipatia halmashauri hiyo kiasi cha zaidi ya milioni 30 kwaajili ya ujenzi wa uzio wa shule hiyo na kwamba ujenzi wake unatarajia kuanza haraka iwezekanavyo.
"Waheshimiwa wajumbe naomba niwaondolee wasiwasi wa hilo...serikali kuu tayali imeshatupatia zaidi ya milioni 30 kwaajili ya ujenzi wa uzio wa shule ya msingi Chato na ujenzi huo tunatarajia utaanza hivi karibuni"amesema Manunga.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Bwanga, James Kahola, ameiomba halmashauri hiyo kujenga uzio kwenye kituo cha afya Bwanga ili kunusuru maisha ya watumishi pamoja na kunusuru mapato ya serikali kutokana na baadhi ya wagonjwa kutoroka wodini pasipo kulipia gharama za matibabu waliyopokea baada ya kulazwa hapo.
Mwisho.



Post a Comment