***********
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) leo wamekutana na wadau kukusanya maoni kuhusiana na kanuni mpya zilizotungwa chini ya sheria ya usafiri majini kwa ajili ya kutekeleza mikataba ya kimataifa.
Akifungua kikao hicho Jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar Khadija Rajabu amesema katika kikao hicho pia watafanyia kazi mapungufu 20 ambayo kwa mujibu wa miongozo ya IMO mapungufu hayo yanatakiwa kufanyiwa kazi ndani ya miaka mitatu tangu ripoti ya ukaguzi kutolewa tarehe 24 nwezi wa 6/2020.
Aidha amesema kupitia kitengo cha sheria cha TASAC kilitakiwa pia kupitia mapungufu ya vipengele vya kanuni za TASAC yaliyoanishwa kwenye ukaguzi katika mikataba 6 ambayo Tanzania imeridhia ikiwemo mkataba wa usalama wa maisha baharini, kuzuia uchafuzi wa mazingira baharini utokanao na shughuli za meli, viwango vya mafunzo vyeti na ukaguzi wa mabaharia, mstari wa ukomo wa upakiaji wa meli, upimaji wa ukubwa wa meli na mkataba wa kuzuia mgongano baharini.
Ameongeza kuwa TASAC imeendelea kuboresha huduma zake kwa kuwa na kanuni madhubuti za kusimamia usafiri wa majini katika nchi zinazopendekezwa kufungwa na kanuni zinazofanyiwa marekebisho ambapo kanuni hizo mpya ni pamoja na kanuni ya ubebaji wa shehena ya michele na mafuta ya mwaka 2023, kanuni ya uchafuzi wa mazingira majini, usafiri majini na ubebaji wa bidhaa hatarishi zote za mwaka 2023.
Hata hivyo amesema kanuni zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni pamoja na kanuni za ukaguzi wa meli za kigeni baharini ya mwaka 2023 na kanuni za kuzuia uchafuzi utokanao na mafuta ya mwaka 2023 zilizoainishwa chini ya sheria ya usafiri wa majini sura ya 165 ambayo imependekezwa kufutwa na kuandikwa upya.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu TASAC Moses Rajabu Kabamba amesema wanachokifanya ni kutekeleza maangalizo na mapungufu ambayo ni maagizo ya Makatibu Wakuu wa Wizara za Sekta ya Uchukuzi za Serikali ya Muungano na Zanzibar.
Amesema wanapokea maoni ya kanuni 6 ambazo zimetengenezwa ili zikakasaidie masuala ya usafiri wa majini na kuondoa mapungufu yaliyotambuliwa wakati wa ukaguzi na athari zake yasipofanyiwa kazi yanaweza kusababisha meli za kimataifa kuzuiwa kuingia nchini hivyo ni muhimu kuyashughulikia ukizingatia tunaelekea katika uchumi wa bluu.



Post a Comment