TMA YATOA MWELEKEO WA MSIMU WA KIPUPWE

Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA Dkt Ladislaus Chang’a wakati akitoa taarifa ya Mwelekeo wa Hali ya Hewa kwa kipindi cha msimu wa Kipupwe (Juni hadi Agosti), 2023 
..........................

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania –TMA imesema katika kipindi cha msimu wa Kipupwe kuanzia Mwezi Juni –Agosti mwaka huu hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. 

Pia imeeleza kuwa  hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kusini -magharibi pamoja na ukanda wa Ziwa Victoria. Aidha, vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Juni. 

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA Dkt Ladislaus Chang’a wakati akitoa taarifa ya Mwelekeo wa Hali ya Hewa kwa kipindi cha msimu wa Kipupwe (Juni hadi Agosti), 2023  ambapo amesema kuwa hali ya joto la bahari katika ukanda wa tropiki ya kati ya bahari ya Pasifiki inatarajiwa kuwa ya juu ya wastani, hali inayoashiria uwepo wa El Niño ambayo inatarajiwa kuendelea kuimarika katika kipindi chote cha msimu na hata baada ya msimu. 

Katika Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu) Dkt Chang’a amesema Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13 oC na 19 oC.

 

“Kwa kawaida kipindi cha JJA kinatawaliwa na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, upepo kutoka kusini-mashariki hadi mashariki unatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika Bahari ya Hindi ambao unaweza kusababisha vipindi vya mvua katika maeneo machache ya ukanda wa pwani (mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba)’Dkt Chang’a

Kuhusu athari zitakazojitokeza katika msimu huo, Dkt Chang’a amesema magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, ingawa kwa kiasi kidogo pamoja na vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho na mengine yanayohusiana na hali hiyo.

Mamlaka hiyo pia imewashauri wakulima katika kipindi hiko kulima mbogamboga na mazao ya mizizi kama vile viazi katika maeneo oevu na pia katika maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua katika kipindi hiko.

0/Post a Comment/Comments