WALIMU B'MULO WADAIWA KUWEKA BONDI VISHIKWAMBI KWA AJILI YA POMBE

                 


                 
Baadhi ya madiwani wakiwa kwenye kikao chao.
Kushoto ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Leo Rushahu,akiendelea kupokea changamoto za wajumbe wa baraza hilo,akiwa na Katibu wa kikao,Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Inacent Mkandara.
*********

Na Daniel Limbe,Biharamulo

BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera,limesikitishwa na baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari kuweka bondi vishikwambi kwaajili ya kulipia pombe kwenye vilabu (Bar) jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Mbali na hilo,pia imeelezwa kuwa baadhi ya walimu wamekuwa wakizurula mtaani kutwa nzima na vishikwambi hivyo,huku baadhi yao wakivihonga kwa wapenzi wao na wengine wakivitumia kupiga picha makanisani na kwenye sherehe za harusi.

Hayo yameibuliwa leo mei 5 kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo ambapo diwani wa kata ya Nyantakara,Sospeter Rugula, amesema baadhi ya walimu wake wamewapatia wapenzi wao vishikwambi vya serikali jambo ambalo linampa mashaka iwapo walipewa elimu ya nyaraka hiyo kabla ya kukabidhiwa.

Kadhalika amewaomba maofisa elimu Msingi na Sekondari kuwaelimisha walimu kuacha kuzurula na nyaraka hizo mitaani hali inayochangia baadhi yao kuziweka bondi kwenye vilabu vya kuuzia pombe kinyume na lengo la serikali la kuwapatia vifaa hivyo.

Diwani Kata ya Ruziba,Athanas Sumbuso,amedai kuwa baadhi ya walimu wilayani humo wamekuwa wakivitumia vishwambi hivyo kutafutia wapenzi badala ya kuonekana wakiwa na simu za vitochi.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu, amekemea vikali vitendo vya walimu kuweka bondi vishikambi kwaajili ya pombe huku akitupa lawama kwa baadhi ya walimu ambao wamekuwa na tabia ya kwenda kunywa pombe muda wa mapumziko ya saa nne asubuhi kwa madai kuwa hilo ni kosa kisheria.

Hata hivyo amekiri kuwepo kwa taarifa za baadhi ya walimu kunyang'anywa vishikwambi hivyo kwa sababu ya madeni ya pombe huku akiagiza watendaji kuwaelimisha walimu hao na kwamba iwapo hawatabadilika wapigwe picha na ziwasilishwe kwenye mamlaka za kinidhamu.

"Lazima walimu wetu watambue kuwa vishikwambi walivyopewa hizo ni nyaraka muhimu za serikali...huwezi kuwa na nyaraka kama hiyo halafu unazunguka nayo kwenye vilabu vya kunywea pombe kwa kisingizio eti ndipo kuna patikana mtandao...hili halikubaliki na ninawaonya wote wanaofanya hivyo" amesema Rushahu.

                      Mwisho.

0/Post a Comment/Comments