LHRC YATAKA MABADILIKO BAADHI YA VIPENGELE MKATABA WA BANDARI


**********

KUFUATIA mijadala mbalimbali juu Mkataba baina ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai wenye lengo la kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika uendelezaji wa maeneo ya Bandari nchini, kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC kimeishauri serikali kufanya mapitio kwa baadhi ya vipengele vyenye changamoto za kisheria ili kuwezesha mkataba huo kuleta tija iliyokusudiwa kwa jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga amesema kituo hiko kimefanya uchambuzi wa mkataba huo kwa mtazamo wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na uwazi, uwajibikaji na dhana ya ushirikishwaji wa wananchi katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi.

Aidha wakili Henga amesema kuwa katika uchambuzi huo kituo kimebaini maeneo yaliyozua mijadala maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na aina ya uwekezaji, mchakato wa manunuzi, faida inayotarajiwa kupatikana, suala la motisha na kodi, uimara wa mkataba, muda wa ukomo wa mkataba husika pamoja na utatuzi wa migogoro.

Vilevile amesema kuwa LHRC inapendekea mkataba wa utekelezaji kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kupitiwa na kukubaliwa kwa maslahi ya umma kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi huku akiwataka wadau wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni chanya yatakayosaidia kupata uwekezaji wenye tija kwa uchumi wa watanzania na nchi kwa ujumla.

0/Post a Comment/Comments