MWENYEKITI UWT NJOMBE AWATAKA WAZAZI KUSIMAMIA MALEZI YA WATOTO







****

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT)Mkoa wa Njombe  Scholastica Kevela amewataka wazazi nchini hususani kina mama  kurudi katika misingi ya malezi bora kwa watoto ili kupunguza vitendo  visivyo na maadili katika jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kikundi cha 'Binti CCM' kilichoanzishwa chini ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Ludewa, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe Scholastica Kevela amesema katika kipindi cha hivi karibuni kumejitokeza vitendo vya mahusiano ya jinsia moja jambo ambalo ni kinyume na maadili ya Tanzania.

Mbele ya wazazi, walezi wanafunzi  walioudhuria katika uzinduzi huo, Mama Kevela amesema  baadhi ya wazazi  hivi sasa wamejiekekeza katika kutafuta vipato na kuyaacha majukumu ya malezi kwa ndugu au wazaidizi wao wa kazi na  kupelekea watoto kukosa misingi ya malezi bora na hivyo  kujiingiza katika vitendo visivyofaa.

"Tunatambua kuwa kila mtu lazima ajishughulishe ili kujipatia kipato lakini ni vyema pia kuhakikisha kuwa malezi ya watoto yetu tunayapa kipaumbele, wengi wetu siku hasa wakina mama tumegeuka na kujipa majukumu ya wanaume na kuacha kufuatilia mwenendo wa watoto wetu" amesema Mama Kevela

Pamoja na wazazi pia Mwenyekiti huyo wa UWT amewaasa wanafunzi walioudhuria uzinduzi huo na wengine wote nchini hususani wasichana kuepukana na mahusiano na zaidi waelekeze akili zao katika masomo ili kujijengea misingi bora kwa ajili ya maisha yao ya baadae.

Aidha mbali na hilo akizungumza katika uzinduzi huo Mama Kevela pia amekemea vitendo vilivyokithiri vya ukatili kijinsia katika jamii na kumtaka kila mwananchi katika jamii kuwa Balozi wa kupinga vitendo hivyo kwa kuwa vinaathiri mwenendo wa maisha katika jamii.

Mama Kevela ambaye ni mjumbe wa Baraza la Taifa la kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, amesema ni wazi kuwa ukatili wa kijinsia unajitokeza katika maeneo mengi nchini hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anapambana navyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Ludewa Hellena Msanga pamoja na kumpongeza Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe Scholastica Kevela amewasisitiza wazazi kuhakikisha suala la malezi ya watoto linapewa kipaumbele. 

Amesema jukumu la malezi kwa watoto linabaki kuwa namba moja kwa kila mzazi hivyo vyema kila mmoja kutimiza wajibu wake katika usimamizi wa malezi ya watoto suala  ambalo linajenga msingi wa maisha bora  na yenye misingi ya kumlinda kimaadili.

Ends

0/Post a Comment/Comments