Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Leo Rushahu,akizungumza kwenye kikao cha madiwani.
Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo.
Katibu tawala mkoa wa Kagera,Toba Nguvila,akizungumza na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo wakiendelea kujadili hoja za CAG.
******
Na Daniel Limbe,Biharamulo
WAKATI rais Samia Suluhu Hassan akiendelea kupanga safu za viongozi mbalimbali serikalini wakiwemo wakuu wa mikoa kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi, katibu tawala mkoa wa Kagera,Toba Nguvila,ameonekana kuujadili uteuzi wa Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam,Albert Chalamila.
Ni baada ya kudai kuwa uteuzi wa Chalamila,ni sawa na kupanda cheo kutokana na awali kuhudumu kwenye mkoa wa Kagera ambao una watu takribani milioni 2.9 ukilinganisha na mkoa wa Dar es salaam ambao una watu zaidi ya 6,000,000.
"Kwangu mimi hii nachukua kama ni kupata promosheni maana yake ni kwamba yeye, sisi na nyinyi tulifanya kazi nzuri ndiyo maana akaonekana...tusinge fanya vizuri naamini wakurugenzi wa halmashauri msinge kuwepo kwenye nafasi zenu...wakurugenzi wa halmashauri zote nane hakuna hata mmoja aliyepoteza kibarua chake".
"Lakini mmesikia wakurugenzi zaidi ya 25 wamepumzika sasa ukiangalia kwa umakini ni kwamba kuna kazi kubwa imefanyika kwenye mkoa wetu"amesema Nguvila.
Alikuwa kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera kilichoketi kwa lengo la kujadili hoja za Mdibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG).
Katika hatua nyingine, Nguvila amewaagiza madiwani wa halmashauri ya Biharamulo kuwachukulia hatua kali watumishi wote waliosababisha kupatikana kwa hoja za CAG kwenye wilaya hiyo na kwamba wasione aibu wala kufumbwa midomo katika kuchukua maamuzi magumu.
Aidha amesema chanzo cha hoja hizo ni baadhi ya watumishi kufanya kazi kwa mazoea, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi na maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.
Mbali na kumpongeza rais Samia kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu,amesema wataendelea kusimamia vyema fedha za halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nidhamu ya kazi kwa watumishi wote wa umma.
Sambamba na hilo,amesema halmashauri yake imeendelea kujibu hoja za CAG na kuzifunga,jambo linaloongeza ufanisi wa kazi kwa watumishi na madiwani kwa ujumla.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Innocent Mukandala, amesema takribani miaka mitatu mfululizo wamefanikiwa kupata hati safi ya ukaguzi wa CAG na kwamba watahakikisha wanaendelea kufanya kazi kwa maadili na uzalendo ili kuwasaidia wananchi kupiga hatua za kimaendeleo haraka zaidi.
Mwisho.



Post a Comment