SERIKALI KUHAKIKISHA FILAMU ZINAZO ZALISHALISHWA NCHINI ZINAKUWA NA VIWANGO VYA KIMATAIFA.






*********

Na Lilian Ekonga

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema serikali kwa kushirikiana na sekta ya filamu nchini watahakikisha kuwa filamu zinazozalishwa hapa nchini zinakuwa na viwango vya kimataifa ili kuwa na ushindani na filamu Duniani

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa filamu ya kisayansi (Sci-Fi) inayoitwa EONII ambayo imetayarishwa na kufadhiliwa na Azam Media Group na Kampuni ya Power Brush amesema kwa sasa sekta ya filamu inapiga hatua kubwa ambapo barani Afrika, Tanzania ni ya pili kwa filamu nyingi ambazo zinazalishwa ikitanguliwa na Nigeria.

Aidha amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya filamu nchini kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania ambao miongoni mwa wanufaika wa mfuko huo ni wasanii wa filamu ili kuboresha kazi zao ziwe na kiwango cha kimataifa.

“Maeneo ambayo yamenufaika na bilioni 1 ambayo imetolewa na Serikali ni sekta ya filamu, na tunatarajia kutoa bilioni 1.7 ambazo zitakuwa zikiongezeka kadiri bajeti itakavyoongezeka” amesema Katibu Mkuu Bw. Yakubu.


Kwa upande wake Mwandaaji wa filamu ya EONII, Eddie Mzale amesema Filamu hiyo ni ya kihistoria kwa kuwa ni filamu ndefu ya kisayansi iliyotengenezwa hapa nchini na maudhui yake yanalenga jinsi teknolojia itakavyotatua changamoto za kijamii kwa miaka ijayo (2061 na kuendelea).

Naye Mkuu wa Chaneli ya Sinema zetu kutoka Azam Sophia Mgaza amesema kupitia filamu hiyo watahakikisha kuwa ionekana katika ubora wake kutokana na uwekezaji uliofanyika na bado wanaendelea na uzalishaji wa filamu nyingine bora zaidi.

Hata hivyo filamu hiyo utaendelea kuonyeshwa kwenye mikoa mingine ikiwemo Dodoma, Tanga, Arusha, Mwanza na Zanzibar ambapo wananchi wameombwa kujitokeza kwa wingi kuitazama filamu hiyo.

0/Post a Comment/Comments