TAARIFA ZA SENSA ZITUMIKE VYEMA KWA MASLAHI YA WOTE - MHE. OTHMAN









 *****


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema taarifa za Sensa ni fursa kubwa kwa Mamlaka na Taasisi za Serikali, katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo kwa jamii na Taifa zima.  

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo huko Ofisini kwake Migombani Jijini hapa, akipokea Ripoti ya Sensa ya Watu na Makaazi ya Mwaka 2022, kutoka kwa Ujumbe wa Kamati Maalum ya Takwimu Zanzibar.

Ujumbe huo ulioongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango, Dokta Saada Mkuya Salum, umewajumuisha pia Kamisaa wa Sensa Nchini, Balozi Mohamed Hamza, na Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar, Bw. Salim Kassim Ali.

Amesema kama ambavyo zoezi hilo la Mwaka jana lilivyofanyika kwa ufanisi wa hali ya juu kutokana na teknolojia iliyotumika ikizingatia kila vigezo vya uwiano (parameters), ni fursa kwa Watendaji na Wasimamizi wa Taasisi mbali mbali za Serikali, kutumia taarifa hizo muhimu katika utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo.

Mheshimiwa Othman ametolea mfano Taarifa juu ya Anuani za Makaazi (Post Codes), akisema kuwa zikitumika vyema na kuzidisha uelewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa Ripoti ya Sensa kwa Maendeleo, zinaweza kuleta tija, hasa kwa kuzingatia kwamba sehemu ya utajiri mkubwa katika ulimwengu wa sasa, ipo katika ’data’ na Takwimu.

Aidha, Mheshimiwa Othman amehimiza matumizi ya Ripoti hiyo ya Matokeo ya Sensa ili kuhakikisha Sekta Binafsi inajumuika ipasavyo katika  kusaidia kujenga mwamko wa matumizi ya taarifa muhimu na kuhamasisha ushiriki wa maendeleo kwa jamii yote.

Hivyo amebainisha na kuishauri Wizara inayohusika na Fedha na Mipango kwamba inalo jukumu kubwa la kuhakikisha inakaa na kuona ni vipi Taarifa hizo Muhimu, kwa upande wa Taasisi za Serikali zinaweza kuzifanyia kazi katika kufanikisha mambo mengi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais wa Zanzibar, Fedha, Uchumi na Mipango, Dokta Saada Mkuya Salum, amesema kwamba ni dhahiri kuna kazi nzito ya kuihusisha na kuijengea uelewa jamii kwa upana wake juu ya umuhimu wa Taarifa za Sensa katika maendeleo na maisha yote, ingawa kwa kuona hilo hata Hotuba yake ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha wa 2023 – 2024 hivi karibuni katika Baraza la Wawakilishi imelizingatia.  

Naye, Kamisaa wa Sensa Nchini, Balozi Mohamed Hamza, amesema kuwa Zoezi la Usambazaji wa Ripoti ya Sensa kupitia Njia mbali mbali limeanzia Ngazi za Juu za Kitaifa, kuelekea daraja za chini na huko ndiko ambako uhamasishaji hasa utaihusisha jamii ili kuleta manufaa zaidi; bali suala la utekelezaji wa Taarifa hizo halina budi, kwa kuzingatia Mwongozo ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan, alishauwasilisha wakati wa Uzinduzi wake.

Wakati huo huo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amekutana na kuwasilisha Maoni yake mbele ya Ujumbe wa Uongozi wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, kuhusu Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2004.

Ujumbe wa Uongozi huo ambao umekuwa ukikusanya maoni ya Kitaalamu kutoka Mamlaka na Taasisi mbali mbali Nchini, juu ya Kuifanyia Mapitio Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2004,  umeongozwa na Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti, kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Maryam Issa Juma.


Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Juni 07, 2023.

0/Post a Comment/Comments