Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dokta Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa dhamira yake ya Uanzishaji wa Mfuko wa Hijja hapa nchini ili kuwawezesha waislamu wengi zaidi kupata fursa na uwezo wa kwenda kutekeleza Ibada hiyo
Alhaj Dokta Mwinyi ameeleza hayo leo, kupitia Hotuba yake ya Baraza la Eid el Hajj, iliyowasilishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, huko katika Ukumbi wa Chuo cha Polisi Ziwani, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja.
Amesema katika utekelezaji wa dhamira hiyo njema, Serikali tayari imepokea Ripoti ya Kamati ya Wataalamu ya Kuimarisha Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar, kwa kuiendesha kisasa na kuleta tija zaidi sambamba na kuipa Mamlaka ya kuanzisha na kusimamia Mfuko wa Hijja.
Amesema kuwa mapendekezo ya Ripoti hiyo ambayo utekelezaji wake utaanza hivi karibuni, yamezingatia upeo mkubwa zaidi wa shughuli za Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, zikiwemo uanzishaji na usimamizi wa Mfuko wa Hijja; Usimamizi wa Nguzo ya Zakka; Uratibu wa ‘Baytul-maal’, Ibada ya Umra; na Ziara au Utalii wa Kiislamu; na hivyo katika kufanikisha hayo, yawapasa Waislamu na Wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa na subira pamoja na kuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu Aliwafikishe jambo hilo.
Aidha Mheshimiwa Dokta Mwinyi ameipongeza Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana kwa mashirikiano yao ya karibu na Taasisi za Hijja Zanzibar, katika kuuelimisha umma juu ya umuhimu wa kwenda kuitekeleza Ibada hiyo adhimu, kwa mwenye uwezo, na kuratibu Safari za Mahujaji, hali ambayo imechangia ongezeko la Mahujaji.
Akibainisha sehemu ya kuhamasisha utekelezaji wa dhamira hiyo, Alhaj Dokta Mwinyi amefahamisha kuwa tayari makubaliano yameshafikiwa na Serikali ya Saudi Arabia ya kuwa na akaunti mbili za kielektroniki katika uendeshaji wa shughuli za Hijja chini ya Ofisi moja (Biitha) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dokta Mwinyi amesisitiza hayo kwakusema, "Kadhalika tunayo matarajio makubwa kwamba Shirika la Ndege la Saudi Arabia litaanzisha safari zake moja kwa moja kutokea uwanja wetu wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume. Hapana shaka, kuanza kwa safari hizo kutawapa fursa Mahujaji kuweza kusafiri kwa wepesi na gharama nafuu".
“Ni matarajio yangu kuwa idadi ya Mahujaji kutoka Zanzibar na Tanzania kwa jumla itaendelea kuongezeka kila mwaka hasa kutokana na jitihada za pamoja zinazochukuliwa za kuzitatua changamoto ziliopo katika utekelezaji wa Ibada hii”, ameongeza Dokta Mwinyi.
Kwamujibu wa Hotuba yake hiyo amesema ni jambo la kushukuru kuona Mahujaji kutoka Zanzibar Mwaka huu wameongezeka, ukilinganisha na idadi ya Mahujaji waliohiji mwaka jana ambao ni 1599.
Amebainisha ongezeko hilo akisema kuwa kwa Mwaka huu wa 1444 Hijriya, Taasisi za Zanzibar zimeweza kusafirisha jumla ya Mahujaji 2133 kati ya 3069 waliokwenda kuhiji kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Dokta Mwinyi ametoa wito kwa jamii kuzingatia na kutekeleza mafunzo yanayotokana na Ibada ya Hijja akisema,“Hija ni mithili ya taasisi ya mafunzo ya malezi na maarifa kwa Waislamu katika misingi ya tawhidi kwa kumtukuza Mwenyezi Mungu na huanza kwa kuweka nia na ikhlasi. Mafunzo haya yana mchango muhimu kwa mja kuwa mcha Mungu kwa kujiepusha na vitendo vyote vitakavyomtoa katika njia ya Mwenyezi Mungu na mafunzo ya Bwana Mtume Muhammad (SAW) aliyeletwa kwetu kutupa miongozo”.
“Jambo jengine muhimu tunalojifunza katika Ibada ya Hija ni kubainisha hisia za Umoja wa Kiislamu na usawa wa wanaadamu mbele ya Mwenyezi Mungu; Waislamu kutoka mataifa mbali mbali, wenye nyadhifa, uwezo na rangi mbali mbali hukusanyika pamoja katika mji mtukufu wa Makka na Madina, wakiwa na lengo moja la kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu wa kufanya ibada katika nyumba tukufu ili kupata uongofu”, amesema Alhaj Dokta Mwinyi.
Amefahamisha kuwa ni faraja iliyoje kwa Muislamu kupata wasaa katika uhai wake kujumuika katika mkusanyiko mkubwa wa Umoja wa Waislamu wa kila mwaka katika nyumba tukufu na kwamba kwa mazingira hayo mahujaji hupata fursa ya kujadiliana masuala mbali mbali ya maendeleo na namna ya kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili katika ulimwengu wa leo. Kama ambavyo Ibada ya Hijja ni kielelezo cha umoja, udugu na mshikamano, Alhaj Dokta Mwinyi amesema ni matarajio kwa Mahujaji kurudi kuyatekeleza na kuyaendeleza mafunzo hayo ili Nchi izidi kubaki katika amani, utulivu na hatimaye kupata mafanikio yakiwemo ya ustawi wa uchumi na kukuza maendeleo ya jamii.
“Kwa hivyo, kwa kuwa hali hiyo ya umoja na mshikamano, mtu anaweza kuihisi katika wiki chache tu za kukutana na watu kutoka nchi mbali mbali kwa mamilioni wakati wa Hija, ni vyema akaiendeleza wakati anaporudi hapa nyumbani tunapoishi siku zote; hiyo itakuwa ndiyo namna bora ya kuyatumia mafunzo hayo yanayotakiwa yadumu katika maisha yetu ya kila siku na ndiyo kielelezo bora cha mtu aliyekwishahiji”, amesema.
Akisisitiza suala la amani, Mheshimiwa Dokta Mwinyi amesema,“napenda nisisitize kwa mara nyengine tena kuhusu suala la kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu”.
Aidha Mheshimiwa Dokta Mwinyi amefahamisha kwamba Nchi inasherehekea Eid wakati ambao zipo harakati za matengenezo makubwa ya barabara, Mijini na Vijijini, hali ambayo inaweza kusababisha usumbufu katika upatikanaji wa huduma mbali mbali zikiwemo za usafiri wa barabarani, na hivyo kuzitaka taasisi za Serikali zikiwemo Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) na Shirika la Umeme (ZECO) kufanya kazi kwa karibu na wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa barabara ili kupunguza athari zinazotokana na harakati hizo.
“Kadhalika, niwaombe wananchi kuwa wastahamilivu kutokana na athari zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara kwa kuamini kuwa hali hii ni ya mpito na ina manufaa makubwa na faida nyingi kwetu sote baada ya kukamilika kwake. Serikali inaendelea kuwasimamia wakandarasi ili kuhakikisha kazi yao inamalizika kwa muda kulingana na mikataba na miradi hii ya ujenzi inakuwa na viwango bora na itakayodumu kwa muda mrefu”, ameongeza Dokta Mwinyi.
Pamoja na kuhimiza na kupongeza juhudi mbali mbali za kusherehekea Eid kwa furaha, ambayo imeonekana hata ndani ya Maeneo hayo ya Jeshi la Polisi wakati wa Hafla hiyo, Alhaj Dokta Mwinyi ameitaka Jamii uiendelee kuwaombea dua Mahujaji, Mwenyezi Mungu Awarudishe nyumbani kwa salama na afya njema, sambamba na kuiombea Nchi izidi kubaki katika hali ya amani, utulivu, umoja na mshikamano, ili kupiga hatua zaidi za maendeleo.
Kabla ya Hotuba hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman, ameeleza shukran zake za dhati kwa niaba ya wahusika wote, wakiwemo masheikh, kutokana na ufanikishaji wa Shughuli hiyo na hatimaye kumkaribisha Mgeni Rasmi ili awahutubie wananchi.
Mawaziri, Viongozi mbali mbali wa Serikali, Dini, Mabalozi na Wanadiplomasia, Vyama vya Siasa, Wawakilishi wa Jumuiya za Kimataifa, Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Asasi za Kiraia, wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, wamehudhuria katika Hafla hiyo.
Wengine waliohudhuria ni Sheikh Saleh Omar Kaabi (Mufti Mkuu wa Zanzibar); Dkt. Amani Abeid Karume (Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita wa Zanzibar); Dkt. Ali Mohamed Shein (Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba wa Zanzibar); Mhe, Zubeir Ali Maulid (Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar); Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (Jaji Mkuu wa Zanzibar); Sheikh Hassan Othman Ngwali (Kadhi Mkuu wa Zanzibar); na Mhandisi Zena Ahmed Said (Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi).
Hafla hiyo imeambatana na Vitendo na matukio mbali mbali yakiwemo Dua, Usomaji wa Qur-an Tukufu na Maelezo yake, Dhifa, pamoja na Qaswida kutoka kwa Wanamadrassa.
Sikukuu ya Eid el Adh-ha inakuja kufuatia Waislamu kutoka Ulimwenguni kote, kukamilisha Ibada ya Hijja, Nguzo ya Tano ya Dini ya Kiislamu,huko Makkah, Nchini Saudi Arabia.


Post a Comment