WADAU WA HUDUMA ZA UONGOZAJI NDEGE NCHINI WAKUTANA KUJADILI MABORESHO YA UTOAJI WA HUDUMA HIYO MUHIMU


             *****

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amefungua mkutano wa wadau wa huduma za uongozaji ndege nchini uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere  jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Mhe. Mwakibete ameipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania kwa kuandaa mkutano huu unaowaleta pamoja wadau wote muhimu wa huduma za uongozaji ndege ambapo kwa pamoja wanajadili na kuja na maazimio yatakayoboresha utoaji wa huduma hiyo.

"Nimefarijika sana kuwaona ninyi ambao ndio wadau wa huduma hii yenye upekee wake maana hapa imewaona marubani, waongozaji ndege, wahandisi wa mitambo ya kuongozea ndege, watoa taarifa za usalama wa anga, Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja nanyi kampuni za ndege. Hii ni ishara njema kwetu kama serikali kuwa mnayo nia moja ya kuhakikisha anga letu linahudumia kisasa na kwa umoja, hivyo serikali ipo nanyi katika masuala yote mtakayojadiliana kwenye mkutano huu”. amesema Mhe. Mwakibete

Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Daniel Malanga aliwakaribisha wageni waalikwa kutoka nje ya Tanzania ambao wamekubali na kuitikia wito wa kuja kuhudhuria mkutano huu na kuwasihi kuwa huru katika kubadilishana uzoefu na ujuzi kwani huduma za Uongozaji Ndege zinategemeana.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Uongozaji Ndege wa TCAA Flora Mwanshinga amesema mkutano huu unawaleta wadau wa huduma za uongozaji ndege nchini ili kujadili changamoto, maboresho, teknolojia mpya kwa lengo la kuboresha utendaji wa kila mdau anayetoa huduma.

Mkutano huo wa siku mbili ni sehemu ya jitihada za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania katika kuhakikisha huduma za uongozaji ndege zinazidi kuboreshwa ili kuendelea kuhudumia wadau wa sekta kwa ubora wenye  viwango vya kimataifa.

0/Post a Comment/Comments