ITILIMA YATENGEWA MILIONI 795 ZA DAWA MWAKA 2023/2024







"""""""""

Na. WAF - Itilima, Simiyu

Wilaya ya Itilima imetengewa fedha za ununuzi wa dawa kiasi cha shilingi milioni 795 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ukilinganisha na shilingi milioni 127 kwa mwaka wa fedha 2020/21.

Hayo yameelezwa leo Julai 11, 2023 na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Itilima, kituo cha afya Nkoma pamoja na Zahanati ya Luguru Wilayani Itilima.

Waziri Ummy amesema fedha hizo za dawa zimeongezeka kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za dawa na hivyo kufanya dawa hizo kupatikana kwenye vituo vya kutolea huduma.

"Katika mwaka wa fedha  Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mara ya kwanza imeongeza fedha za bajeti ya dawa kwa Mwaka 2023/24 kutoka Mil. 127 mwaka 2020/21 mpaka Mil. 795 Mwaka 2023/24, kwa hili Rais ametimiza wajibu wake kwa kutuletea fedha za dawa kwa asilimia 100.

Aidha, Waziri Ummy ameridhishwa na utolewaji wa huduma katika Hospitali ya Wilaya Itilima na ametaka uongozi wa Wilaya hiyo kuweka mazingira rafiki kwa wataalamu wa afya ili wabakie na waendelee kutoa huduma bora kwa Wananchi. 

“Katika Wilaya hii ya Itilima Watumishi wameletwa 37 na Kati yao 36 wameripoti hivyo ni jukumu lenu kama Wilaya kuweka mazingira rafiki ikiwemo kuwalipa posho zao ili vijana hawa waendelee kutoa huduma  katika hospitali hii ya Wilaya”, amesema Waziri Ummy

Wakati huohuo, Waziri Ummy akizungumza na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika Kituo cha Afya Nkoma amesema Wahudumu hao wamesaidia sana katika kuwaibua wagonjwa wa TB 

“Tumegundua kwamba ipo haja ya kuimarisha kada hii ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (Community Health Walkers) kwa sababu ndio wapo karibu na Wananchi”, amesema Waziri Ummy

Amesema, katika kutambua umuhimu wao Serikali itatoa mafunzo  rasmi kwa muda wa miezi Sita kwa watoa huduma hao(miezi Mitatu watakua vyuoni na miezi Mitatu watakua kwenye mafunzo ya vitendo(Field), baada ya mafunzo hayo watapewa posho ya kila mwezi.

“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia amelibeba hili, tunaanza na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 15,000 kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 ambapo katika kila kijiji watakuwepo wahudumu wawili (Mwanamke na Mwanaume)”, amesema Waziri Ummy 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka fedha katika Mkoa huo zaidi ya Mil. 440 kwaajili ya kuboresha huduma ya maji katika Mkoa huo.

“Baada ya kupata fedha hizi tutasambaza maji katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya 40 lakini pia kusambaza umeme katika vijiji ambavyo havina umeme ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Afya kwa Watanzania”, amesema Waziri Ummy

0/Post a Comment/Comments