CHUO cha Taifa cha Usafirishaji kimekuwa moja ya vivutio vikubwa kwa wanafunzi na wazazi mbalimbali katika maonyesho ya 18 ya Vyuo Vikuu yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini(TCU) kutokana na kuvutia na fani mbalimbali za masomo zinazotolewa na chuo hicho kuanzia ngazi ya Cheti hadi Shahada ya Uzamivu.
Maonyesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja ,Dar es Salaam, yamefunguliwa rasmi Jumatatu ya Julai ya 17 na kutarajiwa kumalizika Julai 22 Mwaka huu huku yakivishirikisha Vyuo Vikuu mbalimbali vya hapa nchini na nje ya nchi.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Afisa Mahusiano ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (N.I.T) Juma Manday, amesema kujitokeza kwa wingi kwa wanafunzi kutembelea banda lao lililopo katika Viwanja hivyo kumetokana na kuvutiwa na uwepo wa fani mbalimbali zikiwemo za usafirishaji wa njia za Reli, Anga, Maji na masomo mengine ambayo kimsingi yamelenga kumejenga mhitimu kufanya kazi kulingana na mazingira ya sasa.
Amesema mbali na masomo hayo pia N.I.T hivi karibuni itaanza klufundisha masomo ya Urubani inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu na itagharimu Sh 70 milioni kwa mwanafunzi mmoja.
Amesema kuwa kati ya fedha hizo Sh21 milioni ni gharama za kozi hiyo ngazi ya awali ambayo itamuwezesha mwanafunzi kusoma masomo ya awali na kuruka angani saa 50.
amesema mwanafunzi wa ngazi ya awali akihitimu na kupata leseni yake ya kurusha ndege za watu binafsi atapaswa kuendelea kusoma tena miaka miwili na nusu ili kuweza kupata leseni ya biashara ya CPL ambayo itafanya gharama ya kozi hiyo kuwa jumla ya Sh70 milioni.
"Mwanafunzi huyu akiwa na jumla ya Sh70 milioni atasoma masomo hayo ya awali na hayo mengine yatakayomuwezesha kupata leseni ya CPL ambayo itamuwezesha kuruka saa 200 na kufanya masomo mbalimbali ya hali ya hewa, baada ya hapo muhitimu huyu ataweza kuajiriwa na mashirika ya ndege ya kibiashara ila atatakiwa kuanza na ndege ndogo zenye uwezo wa kubeba abiria 70” amesema Manday na kuongeza kuwa
“Baada ya hapo atatakiwa kusoma tena kidogo ili apate leseni inayoitwa ATPL akipata hiyo anaweza kuendelea kusoma zaidi hadi kufikia hatua ya kuendesha ndege aina ya Dreamliner," amesema
Aidha amesema matumaini kuwa kabla ya mwaka huu kuisha kozi hiyo itakuwa imeanza rasmi hivyo wanafunzi wa kitanzania wataanza kuipata elimu hiyo ya urubani hapa nchini.
Amewataka wanafunzi na Wazazi kuhakikisha wanatumia maonyesho hayo pamoja na dirisha hili na udahili lililotangazwa kuomba nafasi ya kujiunga na Chuo hicho ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kudahiliwa .
“Tunawakaribisha kutembelea banda letu katika maonyesho haya ambapo watapata nafasi ya kufafahamu kozi mbalimbali tunazozifundisha lakini kupitia maonyesho haya pia tutaweza kuwasajili hapa hapa moja kwa moja wakiwa na vielelezo vyao vinavyohitajika ili kuwa na sifa za kujiunga na chuo” aliongeza Manday
ends

Post a Comment