WATU 10 KUTOKA AFRIKA KUSINI WAWASILINI NCHINI KWA AJILI YA MAFUNZO YA UFUGAJI NYUKI

*****

Serikali ya Tanzania imepokea ugeni wa watu 10 kutoka Nchini Afrika Kusini waliofika nchini  kwa lengo la kujifunza juu ya  ufugaji nyuki  hasa kwenye uanzishwaji wa Manzuki na Hifadhi za nyuki, Maandalizi na ukaguzi wa Manzuki pamoja na kuzuia na kudhibiti wadudu kwenye ufugaji nyuki.

Akiongea leo  mara baada ya  Wageni  hao kuwasili,  Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Kamishna Benedict Wakulyamba  amesema ziara hiyo ni ya kimkakati  katika  kuanzisha mazungumzo na  kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini hususan katika eneo la biashara ya mazao ya nyuki, teknolojia za ufugaji nyuki na utafiti.

Amefafanua kuwa  ugeni huo wa Watu 10 unajumuisha Wataalam pamoja na  wafugaji nyuki 


 Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Deusdedith Bwoyo amesema  wageni hao kutoka nchini Afrika Kusini  wamehamasika kuja hapa nchini  kujifunza  namna shughuli za ufugaji nyuki zinavyofanyika.

“Kule Afrika Kusini tumeambiwa  wana uwezo wa kuzalisha tani 2000 kwa mwaka wakati asali inayohitajika ni tani  4000 kwa mwaka, Sisi huku tuzalisha tani  32,691  kwa mwaka na  tunatumia asali hiyo ndani ya nchi  karibia asilimia 90 ” amesema Bwoyo


Ameongeza kuwa " Wamekuja kujifunza ni kwa namna gani tunaweza kuongeza uzalishaji wa asali kule kwao, na pili namna gani wanaweza kuwahamasisha watu kule kwao kutumia asali kama ambavyo sisi tunafanya hii ndio sababu kuu ya ujio wao.


Naye, Kiongozi wa Wajumbe hao ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Maendeleo Vijijini Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini, Zakaria Thupi Mokgathlha, amesema Tanzania ni nchi ambayo imepiga hatua kubwa kwenye eneo la ufugaji nyuki, hivyo wamekuja kujifunza ili waweze kupata ujuzi utakao wasaidia  kujiimarisha kwenye neo hilo.

“ Tumekuja kuangalia Tanzania inavyofanya kwenye eneo hili ili   tutakavyorudi kwetu  tukaweke mikakati ya kuimarisha sekta hii.” amesema Zakaria 


 Katika ziara hiyo, Wataalamu hao watatembelea Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki kilichopo mkoani Tabora  Uongozi wa Mkoa huo pamoja na Vikundi vya wafuga nyuki vya  mkoa huo.

Vilevile, Mara baada ya kuwasili Dodoma wametembelea Ofisi za Manyoni za  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS)  pamoja na Hifadhi ya Nyuki ya Agondi  ambapo wamepata elimu ya namna bora ya kufuga na kuchakata mazao ya nyuki hususani  Asali.

0/Post a Comment/Comments