Na Andrew Chale, Unguja, Zanzibar.
TAHARUKI ilitanda kwa baadhi ya Wananchi wa mji mkongwe wa Unguja, Stone Town kufuatia milio ya fashifashi ama Fataki iliyokuwa ikipigwa kutokea eneo la Forodhani na Darajani, hali ambayo Wageni na wenyeji kuibua hofu kubwa usiku huu.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alikuwa katika moja ya hoteli ameshuhudia baadhi ya Wananchi na Wageni wakipata wasiwasi juu ya milio hiyo ambayo iliibuka ghafla na kuleta tafrani.
Aidha, baadhi ya Wananchi waliamua kukimbilia ndani huku wengine wakipata hofu kubwa wakiwemo wale waliokuwa wamelala na kuamka baada ya milio hiyo.
Hata hivyo, Mwandishi wa Habari hizi, aliamua kufuatilia milio hiyo bila mafanikio lakini aliweza kupata taarifa kutoka katika moja ya chanzo cha ndani kuwa ni utayarishaji wa filamu kuhusu Afya ambayo inaandaliwa na Waigizaji mashuhuri kutoka China ambao wapo Zanzibar kuandaa filamu hiyo.
"Milipo ya fashifashi kutoka kwa Wachina ambao wanatengeneza filamu.
Hofu hii ya watu wengi imekuja kwa sababu leo ama siku mbili hizi hakuna taarifa ya shughuli ya kupelekea kupiga haya mafashifashi," amesema mmoja wa wakazi wa Mji Mkongwe, Salumu Salumu.
Kwa upande wao baadhi ya watu waliokuwa karibu na eneo maarufu la maskani ya watu mbalimbali ya 'Jozi conner' walisema kuwa waliposikia mlio wa kwanza, waliihisi kitu cha kawaida, lakini mlio wa pili na wa Tatu uliwashtua na hata kuhisi kuwa majambazi ama tukio ambalo sio la kawaida hivyo waliamua kutawanyika kabla ya kurejea tena baada kuona ni fashifashi.
"Kipindi hiki hakuna sherehe yoyote, hali hii imetushtua na kuleta sintofahamu.
Kuna watu wameonekana kuchungulia madirishani na wengine kukimbilia majumbani mwao" wameeleza baadhi ya watu.
Hata hivyo imeelezwa kuwa, fashifashi hizo zimeweza kusikika katika sehemu kubwa za Mji wa Unguja, ambapo ziliweza kusikika hata Eneo la Bububu, Darajani, Amani na Mwanakwereke na baadhi ya maeneo.
Awali Mwandishi wa habari hizi aliweza kushuhudia baadhi ya maandalizi ya uandaaji wa filamu hiyo ambapo Wachina hao walikuwa wakichukua vipande eneo chini ya jumba maarufu la Watoto yatima nje ya Ngome Kongwe na eneo la Mizingani Forodhani.
Filamu hiyo inayoandaliwa inaitwa 'MILELE' ambapo inaangazia masuala ya Afya ambayo Taifa la China inafanya katika mataifa mbalimbali Duniani, ambapo kwa mujibu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Wachina hao watafanya filamu hiyo Zanzibar kisha wataenda mataifa mengine katika muendelezo wake, ambapo filamu hiyo pia itasaidia kuitangaza Zanzibar katika masuala ya Utalii.
Taarifa zaidi, kuhusu tukio hilo zinaendelea kuwajia kadri zitakavyopatikana
Mwisho.

Post a Comment