Madiwani wakiendelea na zoezi la kupiga kura ya kumpata makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Biharamulo.
*****
Na Daniel Limbe,Biharamulo
BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera limemchagua Diwani wa kata ya Nemba, Mihayo Lutambi,kuwa makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Lutambi amefanikiwa kutetea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili baada ya kuongoza nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mwaka 2022/23 na sasa ataongoza tena kwa mwaka 2023/24.
Ushindi huo umepatikana huku akiwa mgombea pekee wa nafasi hiyo kutokana na madiwani wote wa halmashauri hiyo kuwa wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo,Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, Inocent Mukandara,amesema uchaguzi huo imefanyika kwa kuzingatia sheria,taratibu na kanuni za kudumu za uendeshaji wa halmashauri nchini na kwamba nafasi hiyo hugombewa kila baada ya mwaka moja.
Amesema jumla ya kura zilizopigwa ni 22 na kwamba kura za ndiyo ni 21 kura ya hapana 1 na hapakuwa na kura iliyoharibika.
"Kwa idhini niliyopewa na mamlaka ninaomba kumtangaza rasmi mgombea kutoka CCM, Mihayo Luganyala Lutambi, kuwa makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Biharamulo baada ya kupata kura za ndiyo 21"amesema Mukandara.
Akitoa salaamu za pongezi baada ya kuchaguliwa tena,Lutambi amewashukuru sana madiwani wote waliomchagua kurejea tena kwenye nafasi hiyo huku akiwaahidi ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha halmashauri hiyo inasonga mbele katika maendeleo yanayokusudiwa.
Aidha amedai atakuwa tayali kushirikiana na madiwani wote pamoja na wataalamu wa halmashauri hiyo huku akiwaomba ushirikiano mkubwa kwa lengo la kuyafikia matarajio makubwa waliyojiwekea.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Leo Rushahu,amewashukuru madiwani kwa kumchagua Lutambi kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa halmashauri hiyo kutokana na ushirikiano mkubwa waliokuwa nao tangu awali.
"Niwapongeze sana kwa kumchagua tena huyu makamu mwenyekiti maana ni mtu ambaye ukimtuma anakubali kutumika...ameniwakilisha vyema sana pale nilipomtaka kufanya hivyo lakini pia mchango wake ulikuwa mkubwa sana kwenye kamati ya fedha,Mipango na uongozi, na matunda yake tumeyaona"amesema Rushahu.
Mwisho.




Post a Comment