DC MATINYI AWATAKA WANANCHI KUTOTUPA TAKA KWENYE MIFEREJI.


 ......................

Na:Joanita Joseph

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Mobhare Matinyi, amewataka wananchi kuweka juhudi katika usafi na utunzaji wa mazingira ili kuokoa fedha nyingi zinazotumika kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa na uchafu badala ya fedha kupelekwa kwenye miradi mingine ya maendeleo.

Mhe. Matinyi ameyasema hayo leo Septemba 11, 2023, wakati akizindua Wiki ya Usafi kuelekea kilele cha Siku ya Usafi Duniani itakayoadhimishwa September 16, 2023.

Mhe. Matinyi amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya usafishaji wa miundombinu iliyochafuliwa na wananchi kwa makusudi wakati fedha hizo zingekwenda kusaidia sehemu nyingine muhimu kama afya, elimu na kadhalika. 

"Mfano mmoja ni mfereji mkubwa wa Serengeti unaopita katika kata ya Keko, uliojengwa kwa Tshs bilioni 18 bila kujumlisha fedha za kuwafidia watu waliobomolewa maeneo yao; Manispaa imetumia milioni 15 kuuzibua na kuusafisha wakati fedha hizo zingeweza kununulia mahitaji hospitalini badala yake tunalipia kijiko kiingie kutoa takataka nje; hii inasikitisha sana," alisema.

Hali kadhalika ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanapendezesha madhari ya Temeke ikiwemo wajasiriamali kuondoka barabarani na kwenda kwenye maeneo rasmi yaliyopangwa kufanya biashara zao. 

Uzinduzi huo umefanyika katika kata ya Kurasini kwenye eneo la Mama na Baba Lishe TRH na kushuhudiwa na Katibu Tawala wa Wilaya Nicodemus Tambo, Mstahiki Meya Abdallah Mtinika, Naibu Meya Arnold Peter ambaye pia ndiye Diwani wa Kata ya Kurasini, Mkurugenzi wa Manispaa, Elihuruma Mabelya pamoja na wakuu wa vitengo na idara wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke

Aidha, wadau mbalimbali wa usafi na kampuni na taasisi kadhaa nao waliungana na wananchi kufanya usafi na baadaye kupata stahafutahi kutoka kwa Mama na Baba Lishe hao waliohimizwa kujali usafi.

0/Post a Comment/Comments