MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imesema itaendelea na mkakati wake wa utoaji elimu kwa Umma kwa kushirikisha wadau wote kwenye sekta ili kuweza kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Bima Tanzania, Dk.Bakayo Saqware wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kupitia mkutano ulioandaliwa na ofisi ya msajili wa hazina Jijini Dar Es Salam.
Amesema mamlaka itaendelea kusimamia kampuni zote za Bima kuhakikisha zinalipa madai na fidia kwa wakati kwa wateja wao wanapopata matatizo ambapo hadi sasa ulipaji wa madai na stahiki umefikia asilimia 95 hivyo kumepunguza malalamiko kwa wateja.
Akizungumzia matarajio yao hadi ifikapo mwaka 2026, Kamishna amesema ni pamoja na kuanza kutekeleza mpango wa kitaifa wa bima ya kilimo pamoja na uanzishwaji wa bodi ya wataalamu wa Bima hifadhi ya jamii na kuweka takwimu za Bima.
Naibu Kamishna wa Bima, Khadija Said, amesema kuhusu mkakati wa utoaji elimu wamejipanga kutafuta mabalozi watakaowasaidia kuelimisha wananchi kuhusu elimu ya Bima kwa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Wahariri Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Deudatus Balile ameishauri Mamlaka kuweka mpango utakaosaidia kukomesha mikopo chechefu au kausha damu kwa kuwa na mfumo wa kukata Bima ili kupunguza usumbufu
Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania ilianzishwa kwa sheria ya Bima ya mwaka 2009 ikiwa na majukumu ya kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima ambapo sekta hii imekuwa kwa asilimia 12.8 kwa mwaka, huku ikiendelea kukua ambapo kwa kipindi cha miaka mitano mauzo ghafi ya Bima yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 691.9 kwa mwaka 2018 hadi Trilioni 1.2 kwa mwaka 2022.


Post a Comment