
..............,..,..
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kipindi cha nusu ya msimu (Novemba 2023 hadi Januari, 2024) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ukilinganisha na nusu ya pili (Februari hadi Aprili 2024), uwepo wa El-Niño unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za Msimu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA na Makamu Mwenyekiti Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia Nchi (IPCC) Dkt. Ladislaus Chang’a, ameeleza hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano na vyombo vya habari kuhusiana na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ambayo ni mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na na Kusini mwa Morogoro.
Dkt. Chang’a amesema kuwa athari zinazoweza kujitokeza ikiwa ni vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, na kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka.
Aidha Dkt Chang’a amesema ongezeko la mvua linatarajiwa katika miezi ya Novemba na Disemba, 2023 huku mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari na Februari, 2024 ambapo amezitaja athari zinazoweza kuchukuliwa na sekta mbalimbali.
Awali Mchambuzi wa Hali ya Hewa Joyce Matwaka ameeleza katika kipindi hicho cha msimu kunatarajiwa kuwepo kwa joto la bahari la juu ya wastani.
Hata hiyo Mamlaka hiyo imetoa ushauri kwa wadau mbalimbali kuzingatia matumizi endelevu ya uhifadhi wa rasimali maji.

Post a Comment