MADIWANI B'MULO WATAKA MADUKA FEKI YA DAWA KUFUNGWA*

Katikati ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Leo Rushahu,kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo na wa kwanza kushoto ni makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Mihayo Miganyalo.
Madiwani wa halmashauri wakiwa kwenye kikao chao.
Diwani wa kata ya Nyarubungo,Petro Kizuluja muda mfupi baada ya kuwasilisha taarifa za maendeleo ya kata yake.

..........................

Na Daniel Limbe, Biharamulo

BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera,limemwagiza mganga mkuu wa wilaya hiyo Dkt. Hamfrey Masuke, kushirikiana na mamlaka ya chakula na dawa nchini ( TMDA) kuchunguza utitiri wa maduka ya dawa za binadamu ambayo yanadaiwa kufunguliwa bila kuwa na usajili.

Hatua hiyo inalenga kunusuru maisha ya wananchi ambao huenda wakapata madhara makubwa kutokana na kuuziwa dawa ambazo hazina ubora uliothibitishwa jambo linaloweza kusababisha usugu wa magonjwa pamoja na vifo.

Kadhalika baadhi ya maduka hayo yanahofiwa kutumia wahudumu wasiokuwa na taaluma ya dawa hivyo kuwepo kwa hatari kubwa ya wagonjwa kupewa dawa zisizostahili.

Uamuzi huo umetolewa baada ya diwani wa kata ya Nyarubungo,Petro Kizuluja,kueleza uwepo wa maduka tisa ya dawa yaliyofunguliwa hivi karibuni kwenye kata yake huku yakiwa hayana usajili unaotambuliwa na serikali kutokana na wamiliki wake kutaka kukwepa ulipaji wa kodi na mapato mengine ya serikali kinyume cha sheria.

Alikuwa akiwasilisha taarifa za maendeleo ya kata yake kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita hali iliyosababisha baraza hilo kutoa msimamo wake haraka ili kunusuru maisha ya wananchi hao.

Akitoa msimamo huo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Leo Rushahu, amemtaka mganga mkuu kuhakikisha anafanya operesheni wilaya nzima na kuyafungia maduka yote yasiyo kuwa na sifa ikiwa ni pamoja na yale yasiyokuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kuuza dawa kama sheria inavyoelekeza.

"Tunakuagiza mganga mkuu wa wilaya(DMO) hakikisha unafanya operesheni kwenye kata zetu zote kukagua maduka yasiyokuwa na sifa kisha uyafunge...na yale yasiyokuwa na wahudumu wenye sifa yafungwe pia...hatuwezi kuacha wananchi wetu wakaumia kwa sababu ya maslahi ya baadhi ya watu wachache" amesema Rushahu.

Hata hivyo mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Inocent Mkandala,amewataka madiwani hao kuongeza ukali katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri hiyo kwa madai kuwa ndiyo msingi mkuu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na wananchi badala ya kutegemea pesa kutoka serikali kuu pekee.

0/Post a Comment/Comments