STAMICO:TUTAENDELEA KUWABEBA WACHIMBAJI WADOGO



**********

Na Mwandishi wetu

Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limesema litaendelea kutoa elimu, vifaa na kuboresha mazingira ya uchimbaji hapa nchini ili rasilimali za Taifa ziweze kusaidia wengi zaidi.

Limesema miongoni mwa mafanikio wanayojivunia ni ushirikiano na makubaliano waliyoingia na benki tano kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo nchini.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa saba wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Ofisa Uhusiano wa shirika hilo, Bibiana Ndumbaro alipokuwa akiwasiliana mada katika Mkutano Mkuu wa saba wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) unaofanyika mkoani Lindi.

Alisema fursa hiyo ya kutoa na kupokea mikopo inalenga kuwawezesha wachimbaji kununua vifaa vya kisasa na kukuza biashara zao, ajira na uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa.

Bibiana alisema makubaliano waliyoingia na benki hizo tano yatawawezesha wachimbaji wadogo kuomba mikopo kwenye taasisi hizo na wao (Stamico) wanapoombwa taarifa wachimbaji hao huzitoa ili wahusika wapate mikopo waliyoomba.

“Kimsingi hapa tunazungumzia benki za NMB, KCB  CRDB na Azania ambazo zipo kusaidia wachimbaji wadogo kufikia malengo yao, rasilimali zetu ni vema zitakatusaidia kupiga hatua kiuchumi” amesema  
Bibiana amesema Stamico imedhamiria kuleta suluhisho la kudumu la upatikanaji wa  mikopo kwa wachimbaji wadogo kwa  kuhakikisha  inasimamia kuanzishwa kwa Benki ya Wachimbaji ambapo taratibu za uanzishwaje wake umeanza.

Amesema kuwa Stamico imeboresha uendeshaji  wa miradi yake na kuifanya kuwa sehemu ya kukusanya mapato na sio matumizi  jambo lililosababisha kuongezeka kwa mapato yake.

“Tumeboresha mradi wetu wa kuzalisha nishati mbadala ya kupikia  kwa kuleta mitambo mikubwa miwili yenye uwezo wa kuzalisha  tani 20 kwa saa kila mmoja ili kuongeza uzalishaji  wa nishati hiyo kuweza kuwafiki wananchi wengi. 

Mitambo hii itafungwa mkoani Pwani na Songwe” amesema 
Bibiana amesema kuwa Stamico imechagiza kuanzishwa kwa kiwanda cha kusafisha dhahabu  cha Mwanza  ambacho  kimechochea ongezeko la thamani ya madini  hivyo kuchochea ukuaji wa ajira na teknolojia kwa Watanzania.

Ameongeza kuwa kupitia  miradi ya ubia Stamico inahakikisha miradi hiyo inarithisha teknolojia na kutoa ajira kwa Watanzania.

Amebainisha kuwa wameendelea kutoa elimu ya teknolojia kwa vitendo kwa wachimbaji wadogo na kuongeza  kituo cha mfano  kwa ajili  ya wachimbaji  wa chumvi  mkoani  Lindi ili kuhakikisha  wanazalisha chumvi yenye ubora kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Mwisho.

 

0/Post a Comment/Comments