********
Wajiolojia kutoka ndani na nje ya nchi wanaoendelea kuwasili Zanzibar wameiishi kwa vitendo ajenda ya utalii endelevu kwa kutembelea maeneo mbalimbali kwa lengo la kutalii na kujifunza zaidi jiolojia ya eneo hilo.
Wajiolojia hao wanaowasili Zanzibar kwa ajili ya mkutao wao wa mwaka utakaofanyika Novemba 09 hadi 11, 2023 Mjini Unguja Zanzibar, wameanza kwa kutembelea Kisiwa cha Changuu, Nakupenda Sandbank na Ngome Kongwe. Ziara itahitimishwa kesho, Novemba 08, 2023 kwa kutembelea maeneo mengine.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wajiolojia wanaoshiriki ziara hiyo wamesema maeneo waliyotembelea na wanayoendelea kutembelea yamewapa kufurahia uwepo wao Zanzibar, kupumzika na kuongeza uelewa wao juu ya jiolojia ya Zanzibar.
Kwa upande wake, mratibu wa ziara hiyo Bw. Japhet Fungo ambaye pia ni Mkufunzi Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kuwa uongozi wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania uliamua kuandaa ziara hiyo kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuhamasisha utalii endelevu kama moja ya maeneo muhimu ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar mwaka 2050.


Post a Comment