HAKUNA UTALII BILA UHIFADHI" DKT. ABBASI

......................

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi Leo Disemba 19,2023 ametembelea sehemu ya Mradi wa Kuboresha Utalii Kusini (Regrow) kwa kufika katika skimu ya Madibira, Mbarali, Mbeya, ambapo wakulima wanaboreshewa miundombinu ya umwagiliaji kuwa ya kisasa ili maji wanayoyatumia yarejeshwe kwenye Bonde la Ihefu na Mto Ruaha Mkuu. 

Dkt. Abbasi amesema hatua hizo si tu zimewasaidia wakulima pembeni  mwa Hifadhi ya Taifa Ruaha na kuongeza mazao lakini tayari pia zimeonesha matumaini ya kuurejeshea uhai zaidi Mto Ruaha Mkuu ambao kwa sasa siku za kukauka kwa mwaka zimepungua.

Dkt. Abbasi ameongeza kuwa  utekelezaji wa mradi wa REGROW Madibira ni  tafasiri kwa vitendo falsafa ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya "Kazi inaendelea" ya  kuwapatia watanzania maendeleo kwa haraka.

Aidha Dkt. Abbasi ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi wa REGROW Madibira sanjari na kuboresha matumizi rafiki ya maji kwa wakulima wa mpunga ili maji yatiririke mto Mkuu Ruaha kwa uhifadhi endelevu  wa Ikolojia na Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Ruaha unakwenda kusaidia upatikanaji wa maji ya uhakika katika Mradi wa Bwawa la kufua umeme la Mwl Nyerere.

"Mto Ruaha Mkuu ni tunu muhimu kwa hifadhi zetu ikiwemo Ruaha lakini pia unachangia asilimia 15 ya maji katika  Mto Rufiji na hivyo ni uhai wa Bwawa la Nyerere". Alisisitiza Dkt. Abbasi.

Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji Madibira,  unaotekelezwa na Mkandarasi  mzawa kampuni ya SkyLine, unaurefu wa takribani kilomita 13 na imekamilika kwa asilimia 95.


 

0/Post a Comment/Comments