TUZO CHA CHEZA KIDANSI ZAWEKA REKODI MPYA




Tuzo pekee za muziki wa dansi Tanzania Cheza Kidansi music awards mwaka 2023 zimefanyika mwisho wa juma hili jijini Dar es Salaam.

Tuzo hizo zimeshuhudia washiriki mbalimbali waliochuana vikali katika vipengele mbalimbali wakikabidhiwa tuzo zao katika ukumbi wa New Kiduli Garden Dsm.

Moja kati ya rekodi kubwa zilizowekwa ni kushuhudia wadau wakubwa walioupigania muziki wa dansi asubuhi na mchana wakikabidhiwa tuzo zao za heshima.

Tukio hilo limepongezwa na mashabiki wengi wa muziki wa dansi nchini kwani limewaenzi wadau hao wakubwa wa muziki wa dansi wakiwa hai.

Wameomba wadau hao waendelee kuenziwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Rekodi nyingine ni ubora wa tuzo za mwaka 2023 ambazo zimeonekana kuwa na ubora mkubwa na mwonekano mzuri unaoendana na ukubwa wa tukio hilo.

Wadau wa muziki wa dansi wakipongeza ubora wa tuzo hizo wameomba iwe fursa kwa wanamuziki kuboresha kazi zao ili kukuza muziki wa dansi.

Rekodi nyingine ni tukio hilo kushuhudiwa na wadau kutoka kada mbalimbali nchini. Tofauti na matukio mengine, tukio hilo limeshuhudiwa na wadau ambao huonekana kwa nadra kwenye matukio ya dansi lakini wakajitokeza kwa wingi kwenye tukio hilo. Wanamuziki wengi wa dansi wa bendi tofauti walijitokeza pia.

Asilimia kubwa ya wanamuziki walioshinda tuzo hizo walikuwepo huku waliokuwa na maonesho mbalimbali wakituma wawakilishi wao kupokea kwa niaba.

Kilio kikubwa cha mashabiki wengi wa dansi cha sound mbovu kilipata muafaka kwani sound ya siku hiyo ilikuwa bora sana na kupongezwa na kila mdau aliyekuwepo ukumbini. Taa pia za jukwaani zilikuwa bora hivyo kufanya kila tukio jukwaani kuonekana vyema kabisa.

Hakukuwepo na tukio lolote la umeme kukata wala hitilafu yoyote ya kiufundi jambo ambalo liliwafurahisha mashabiki wengi waliojitokeza kushuhudia tukio hilo.

Bendi ya Twanga Pepeta ilipata muda wa kutosha wa kutoa burudani jukwaani na kutoa burudani nzito iliyowaacha mashabiki vinywa wazi kutokana na ubora wake. Hata wimbo wa mwisho ulipopigwa na vyombo kuanza kufungwa bado mashabiki walibaki ukumbini wakiendelea kuburudika na kupeana mawazo ya hapa na pale ya tuzo.

Tukio pia la wadau wa muziki wa dansi mbalimbali kupewa fursa ya kukabidhi tuzo limepongezwa na wadau mbalimbali kwani limewapa heshima na kuonekana kuwa sehemu ya ushiriki wao katika dansi.




Kamati tendaji ya CHAMUDATA ikiongozwa na Mwenyekiti Luiza Mbutu ilikuwepo ukumbini ambapo Mwenyekiti huyo aliwaomba wadau wa dansi kusapoti tuzo hizo pekee kwa mustakabali wa muziki wa dansi nchini.

Mwenyekiti mstaafu wa CHAMUDATA Hassan Msumari pia aliwaomba wadau wa muziki wa dansi kuzikumbatia tuzo hizo kwani ni dira ya muziki wa dansi nchini huku akiwausia wanamuziki kuunga mkono jitihada zote zinazofanyika kukuza dansi nchini.

Wadhamini wa tuzo hizo walikuwa Star TV, RFA, Kiss FM, Epic Events, Cheza Kidansi Entertainment, New Kiduli Garden, Shirose Perfumes, K Fabrication, Hillfiger Security, Masaka Transport na wadau wengine.

Washindi Tuzo za muziki wa Dansi Tanzania Cheza Kidansi music awards 2023

Wimbo bora-Mama Mia-Mjengoni Classic Band 

Video Bora-Kanivuruga-Malaika Music Band 

Mtayarishaji Bora-Babu Bomba

Mwanamuziki Bora-Nyoshi El Saadat

Rapa Bora-Baraka Follo

Mwanamuziki Chipukizi-Eric Kato

Mtunzi Bora-Thelathini na Tatu

Bendi Bora-Mjengoni Classic Band

Album Bora-Michimbaki

Mwimbaji Bora wa kiume-Christian Bella

Mwimbaji Bora wa kike-Tabia Batamwanya

Dansa bora wa kiume-Hamza Mapande

Dansa Bora wa kike-Kisura

Mpiga Chombo Bora-Yaniki Solo

Best Collabo-Mwisho wa Ubachela-Sylivia Mwakilufi ft Eric Kato

Mwanamuziki mwenye nidhamu-Digital Mukongya

Wadau Bora

Joseph Alfred Mangapi
Asha Baraka
John Mdenye
Yusuphed Mhandeni
Hamis Kuyega
Hassan Swai
Steve Masaka
Lengos VIP
Patrick Kessy

Mwandishi wa habari Bora-Said Mdoe

Tuzo hizo pekee za muziki wa dansi zitakuwa zikifanyika kila tarehe 9 Disemba siku ya uhuru.





0/Post a Comment/Comments