Na Daniel Limbe, Chato
IMEELEZWA kuwa njia pekee ya kuepukana na mikopo ya kinyonyaji kwa walimu nchini (maarufu mikopo kausha damu) ni kujiunga na huduma za Mwalimu Saccos ili kukidhi mahitaji yao badala ya kwenda kwenye taasisi binafsi za kifedha.
Ni kutokana na baadhi ya walimu kukopeshwa fedha kwa riba kubwa huku baadhi yao wakiporwa kadi za benki na wamiliki wa makampuni ya kifedha, hali ambayo imekuwa ikiwasababishi maisha magumu na kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.
Akiongea na mwandishi wetu Meneja wa Chama cha ushirika cha walimu wilaya ya Chato mkoani Geita(Chato Teachers Saccos), Mwl. Pius Katani, amesema njia pekee ya kuepukana na mikopo ya kinyonyaji ni walimu kutumia chombo chao ambacho ni rahisi kuwasikiliza na kushauriana kwa lengo la kuboresha ufanisi wa maisha tofauti na taasisi zingine ambazo hulenga kujipatia faida pekee.
"Huu ni wakati wa walimu na watumishi wote wilaya ya Chato kuungana pamoja kutumia chombo chetu cha Chato Teachers Saccos ili kuepukana na changamoto ya mikopo kausha damu...maana mikopo hiyo imesababisha baadhi yao kubaki na pesa kiduchu kwenye mishahara yao na hivyo kushindwa kumudu gharama za maisha na kusababisha msongo wa mawazo" amesema Katani.

Post a Comment