MAGEUZI MUHIMU NCHINI,NI KUJENGA MISINGI YA UWAJIBIKAJI-MHE OTHMAN

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa ambao umewashirikisha wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya siasa kujadili muswada wa sheria za uchaguzi na vyama vya siasa ambao umefanyika katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es salaam 
.......................

NA MUSSA KHALID 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman amesema miongoni mwa mageuzi muhimu ambayo nchi inahitaji bila kuchelewa ni kujenga misingi ya uwajibikaji katika ngazi zote.

Makamu wa Kwanza wa Rais Othman amesema hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa ambao umewashirikisha wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya siasa kujadili muswada wa sheria za uchaguzi na vyama vya siasa.

Othman amewasisitiza wadau hao wa kisiasa hasa wenye ujzoefu wa kada tofauti kusaidia kupata mwafaka wa kitaifa ili miswada hiyo inapokwenda bungeni,Wabunge waweze kupitisha jambo ambalo tayari lina mwafaka.

Awali akizungumza Waziri wa NCHI,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge)Jenista Mhagama amesema maoni yatakayotolewa yatachukuliwa kama yalivyo hivyo amewataka wadau kutumia fursa hiyo kwa kutoa maoni yao ili kuweza kuboresha muswada kwa manufaa ya watanzania.

Kwa upande wake Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi amewasisitiza wadau hao wa vyama vya siasa kutoa maoni yao kwani yatachukuliwa yote kwa kuzingatia maandishi.

Baadhi ya wadau wakiwemo vijana katika Vyama vya siasa ambao wamehudhuria katika mkutano huo akiwemo Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana chama cha ACT Wazalendo Abdul Nondo pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Mohamed Kawaida wamepongeza hatua hiyo na kusema inaendana na falsafa ya Rais Samia Suluhu ya 4R.

Mkutano huo maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa unafanyika kwa siku mbili Januari 3 -4 mwaka huu kwa lengo la kutoa maoni ya miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa Bungeni Novemba 10,2023

0/Post a Comment/Comments