SERIKALI YAWEKA MIKAKATI KUZALISHA MBOLEA KWA KUTUMIA MALIGHAFI ZA NDANI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli akizungumza wakati wa kikao cha kujadili Mkakati wa kuzalisha mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Kilimo tarehe 25 Januari, 2025 na kuhudhuriwa na watendaji wa Wizara na taasisi zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa tasnia ya mbolea nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamalaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent (kulia) akifuatiwa na Mkurugenzi wa Kampuni la Mbolea Tanzania (TFC), Samuel Mshote wakifuatilia wasilisho wakati wa kikao kilichokuwa kikijadili Mkakati wa kuzalisha mbolea kwa kutumia rasilimali zinazopatikana nchini tarehe 25 Januari, 2024 Jijini Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao, Upendo Mndeme alipokuwa akifafanua jambo wakati wa kikao kilichowakutanisha wadau wa mnyororo wa thamani wa mbolea kutoka wizara na taasisi mbalimbali katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya kilimo tarehe 25 Januari, 2024

 ...............,............

#TFRA, TFC na GST wasaini Makubaliano (MoU) kutekeleza mpango huo

Katika kuhakikisha mbolea zinazotumika nchini zinazalishwa na viwanda vya ndani, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekuja na mkakati wa kuhakikisha inatekeleza mpango wa kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha mbolea kwa kutumia malighafii zinazopatikana nchini. 

Akizungumza katika kikao kilicholenga kujadili utekelezaji wa mkakati huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Mweli amezitaka Wizara, Taasisi na Mamlaka za Serikali zinazohusika katika utekelezaji wa mpango huo, kuhakikisha maazimio ya kikao hicho yanatekelezeka kwa vitendo na kwa wakati. 

Mafanikio ya mpango huo ni utiaji saini wa Makubaliano hayo ulioshuhudiwa na Katibu Mkuu Mweli ukiingiwa baina ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ukisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) uliosainiwa na Dkt. Leonard Massawe kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa GST, Dkt. Mussa Budeba na Kampuni la Mbolea Tanzania (TFC) uliosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Samuel Mshote.

Makubaliano hayo, yanazipa Taasisi hizo majukumu tofautitofauti kuelekea utekelezaji wa Mkakati huo wa kuzalisha mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini.

Utiaji saini huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Kilimo, Kilimo 4, tarehe 25 Januari 2024.

Akizungumzia umuhimu wa Mkakati huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amesema mpango huo utapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mbolea nje ya nchi* na badala yake fedha hizo zitatumika katika shughuli nyingine za maendeleo nchini.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni la mbolea (TFC), Samwel Mshote amesema, lengo la kusaini makubaliano hayo ni kuangalia namna ambayo taasisi hizo zitashirikiana katika kuhakikisha malighafi kwa ajili ya kuzalisha mbolea kwa soko la ndani na nje ya nchi zinapatikana.

Sambamba na hayo, Mshote amesema, mahitaji ya mbolea ni makubwa ambapo zinahitajika tani milioni moja *ambapo kwasasa ni 10% tu* ndio inazalishwa ndani ya nchi na 90% inaingizwa kutoka nje ya nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa GST, Kaimu Meneja wa Huduma za Jiolojia Bw. Maswi Solomon amesema, GST imeingia kwenye makubaliano hayo kwa lengo la kutafiti na kubainisha maeneo yapatikanayo madini/ malighafi ya kutungeneza mbolea ili kuja na mkakati wa uzalishaji wa mbolea kwa kutumia malighafi hizo.

Pamoja na ushiriki wa Taasisi zilizokuwa zikiingia makubaliano, kikao hicho kilihudhuriwa na wawakilishi wa Makatibu wakuu wa Wizara ya Madini, Wizara ya Nishati, Wizara ya Viwanda na Biashara, watendaji kutoka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).




0/Post a Comment/Comments