Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki amewataka wananchi Kupunguza matumizi ya mkaa na kuni na kutumia nishati mbadala kama mkaa mbadala na gesi ili kunusuru uharibifu wa misitu yetu.
Pia ameelekeza hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa wote watakaobainika kutumia nguvu kwa kuvamia, kudhuru au kuharibu mali za umma.
Waziri Kairuki ameeleza hayo leo jijini Dar es salaam wakati akizindua vitendea kazi vya Doria za misituni ambapo jumla ya vifaa vilivyokabidhiwa ni 43, magari 02 aina ya KAMAZ magari mawili aina ya Land cruiser hard top na pikipiki 39 aina ya Yamaha zenye uwezo wa hali ya juu katika utendaji kazi
Waziri Kairuki amewataka viongozi wa wakala wa huduma za misitu Tanzania kuchukua hatua stahiki kwa Afisa askari wa Uhifadhi wasio na maadili katika kutekeleza majukumu yao.
“Mnatakiwa kufanya kazi kwa weledi na ari ya hali ya juu kwani Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua kazi na dhamana kubwa mliyokabidhiwa” Mhe. Kairuki amesema.
Awali akizungumza Kamishna wa uhifadhi wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS),Profesa Dos Santos Silayo ameelezea utendaji wa taasisi hiyo huku akisema vifaa vilivyozinduliwa vitaimarisha jitihada za usimamizi wa rasilimali misitu na nyuki nchini.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge,ardhi,Maliasili na Utalii Festo Sanga amesema wataendelea kuiunga Mkono wizara na taasisi zake ili iendelee kufanikisha malengo yake.
Kwenye hafla hiyo pia imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TFS, Meja Jenerali Dkt.Mbaraka Mkeremy, Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Menejimenti ya Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania na Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF).
Post a Comment