DKT. ABBASI AHIMIZA KASI UJENZI MIRADI YA REGROW




..................

Na Sixmund Begashe

Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania REGROW, wametakiwa kuhakikisha  miradi ya ujenzi inayoendelea kwenye Hifadhi za Taifa Mikumi inakamilika kwa wakati, na kuwa hakutakuwa na muda utakaoongezwa kwa atakae fanya kazi kwa kusua sua. 

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa miradi hiyo Mikumi Morogoro, kama sehemu ya Kusherekea Miaka miwili Tangu Kuzinduliwa Kwa Filamu ya The Royal Tour.

Dkt. Abbasi amesema kuwa Kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Filamu ya The Royal Tour imeendelea kuvutia Watalii wengi nchini, hivyo mkakati wa kuifungua zaidi kusini kiutalii kupitia mradi wa REGROW unakwenda kuongeza kasi ya utoaji  kuhudumia kwa makundi Makubwa ya watalii watakao tembelea Hifadhi za Taifa Kusini.

Aidha Dkt. Abbasi amempongeza Mkandarasi wa kampuni ya Badr East Africa kutoka Dar es Salaam anaejenga Kiwanja cha ndege Mikumi kwa hatua nzuri aliyofikia hali itakayopelekea kukamilika kwa haraka  utekelezaji wa mradi huku akimtaka Mkandarasi wa Kampuni ya Uniki Construction Engineering (PTY) ya nchini Botswana, anaye jenga Kituo cha Taarifa kwa wageni Hifadhini Mikumi,  kuharakisha ujenzi na kuwa asitegemee kuongezewa muda hivyo afanye kazi bila kujali jua au mvua.

Mradi wa REGROW unaotekelezwa kwa fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, katika Hifadhi ya Taifa Mikumi unatekeleza pia ujenzi wa Mabanda matano ya kulala wageni, eneo la kupumzika wageni, Kambi ya kuweka mahema pamoja na kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia vikundi vya Benki za Kijamii (COCOBA).

0/Post a Comment/Comments