Taarifa zinaeleza kuwa Israel imefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Iran. Miito imetolewa kwa Israel na Iran kujizuia na hatua zozote zitakazopelekea mzozo huo kutanuka katika eneo zima la Mashariki ya Kati.
Vyanzo mbalimbali vinaarifu kuwa leo Ijumaa, Israel imefanya shambulio la kulipiza kisasi katika ardhi ya Iran. Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kwamba milipuko ilisikika katika mji wa katikati mwa Iran wa Isfahan , lakini afisa mmoja Tehran ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba milipuko hiyo ilisababishwa na mifumo ya ulinzi wa anga ambayo ilifanikiwa kudungua droni tatu.
Viongozi wa Israel na hata jeshi la nchi hiyo hawajazungumza chochote kuhusu taarifa hii. Afisa mwandamizi wa Iran ameiambia Reuters kuwa nchi hiyo haina mpango wa kujibu mara moja shambulio hilo, ambalo taarifa kutoka Tehran zinasema halikuwa na madhara makubwa.
Chanzo kinachofuatilia mzozo huo kimeeleza kuwa Marekani ilipokea taarifa kabla ya Israel kufanya shambulio hilo, ambalo linajiri siku chache baada ya Iran kuendesha mashambulizi ya droni na makombora ambayo hayajawahi kushuhudiwa dhidi ya Israel.
Hata hivyo, Shirika la Kimataifa la kudhibiti Nishati ya Atomiki (IAEA) limesema shambulio hilo halijasababisha uharibifu wowote katika miundombinu ya nyuklia ya Iran na kukumbusha kwamba maeneo yenye miundombinu ya nyuklia haipaswi kulengwa katika mizozo ya kijeshi.
cc Dwkiswahili

Post a Comment