***********
Israel
imepeleka vifaru kwenye mji wa Rafah na kutwaa udhibiti wa mpaka kati ya Gaza
na Misri ikiwa ni hatua ya mwisho kabla ya kuanza rasmi mashambulizi yake ya
ardhini yanayopingwa na washirika wake wa Magharibi.
Mapema asubuhi ya Jumanne (Mei 7), jeshi la Israel lilipeleka vifaru
kadhaa kwenye mji wa kusini mwa Gaza, Rafah, ikiwa ni siku moja tu baada ya
kuwaonya Wapalestina wanaoishi huko kuhama kabla ya operesheni ya ardhini
kuanza.
Picha za
vidio zilizosambazwa na jeshi hilo zilionesha vifaru vikipeperusha bendera ya
Israel na vikitwaa udhibiti wa mpaka kati ya Misri na Gaza.
Jeshi la
Israel lilidai kwenye taarifa yake kuwa hiyo ilikuwa ni "operesheni
inayojikita kwenye eneo makhsusi na kwa malengo makhsusi."
Muda mfupi baada ya Israel kutwaa udhibiti wa mpaka huo wa Rafah, Misri iliionya Israel kwamba operesheni hiyo
ilikuwa inatishia juhudi za kusitishwa mapigano, kwa mujibu wa wizara ya mambo
ya kigeni ya Misri.
Umoja wa
Mataifa ulisema Israel inaendelea kuvifunga vivuuko viwili muhimu kwa Ukanda wa
Gaza - Rafah na Kerem Shalom - hatua ambayo imeukatia Ukanda huo uwezekano wa
kupata msaada wowote kutoka nje.
Usiku wa kuamkia Jumanne ulishuhudia mashambulizi makali ya mizinga ya
Israel dhidi ya mji wa Rafah, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa AFP
aliyepo kwenye eneo hilo.
cc DWkiswahili

Post a Comment