Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania-TMA imesema uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi mashariki mwa Pwani ya Mtwara umeendelea kuimarika na kuwa Kimbunga ‘HIDAYA’.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Mamlaka hiyo imesema kuwa kimbunga hicho chenye nguvu ya kati,kikiwa umbali wa takriban Kilomita 506 mashariki mwa Pwani ya Mtwara.
Imesema mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga ‘HIDAYA’ kusogea karibu kabisa na Pwani ya Tanzania kuanzia usiku wa Mei 2,2024 na kuendelea kuwepo hadi tar 6 mwezi huu.
Aidha Mamlaka hiyo imesema Kimbunga hicho kinatarajiwa kupungua nguvu baada ya tar 6 Mei mwaka huu.
Kuhusu athari zinazotokana na kimbunga hicho TMA imesema inatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara,Lindi,Pwani (ikijumuisha visiwa vya mafia)Dar es salaam,Tanga,Morogoro,Visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani.
Mamlaka hiyo imewashauri wananchi tajwa katika maeneo hayo wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini kuchukua tahadhari kubwa pia kuendelea kuafuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka TMA.

Post a Comment