Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo
amesema ajenda ya kutumia nishati safi ya kupikia ni ya muhimu ili kuokoa
maisha ya watu na mazingira.
Amesema
hayo wakati wa mkutano wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bi. Zuhura
Yunus pamoja na viongozi wengine na Vyombo vya Habari, Ikulu jijini Dar es
Salaam leo tarehe 17 Mei, 2024 kuhusu Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia
uliofanyika jijini Paris nchini Ufaransa.
Dkt.
Jafo ameeleza kuwa Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia umefanikiwa kwa asilimia
kubwa chini ya Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika, Rais wa Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na wenyeviti wenza,
wamewezesha upatikanaji wa Dola za Kimarekani bilioni 2.2.
Pia, amesema
Uingereza imeahidi kutoa Dola za Kimarekani 3.4 milioni kwa Tanzania, ambapo ni
mafanikio yaliyopatikana katika mkutano huo ambapo ni fursa kwa nchi katika
kuchagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua itakayowasaidia akinamama
na wasichana kuzalisha na kusoma badala ya kutafuta kuni.
Waziri
Jafo amesema Tanzania imejipambanua katika ajenda ya nishati safi kwa kuwa na
Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao ni nyenzo muhimu
ya kukabiliana na athari za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi.
Amesema
Serikali inashirikisha sekta binafsi katika ajenda ya nishati safi kuhakikisha
uwezo wa wananchi katika kumudu, upatikanaji na kujenga uelewa kwa wananchi
kutumia nishati safi badala ya kuni na mkaa.
Halikadhalika,
amesema maelekezo ya Serikali kwa taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 kuacha
kutumia kuni na mkaa katika kuandaa chakula ni mojawapo ya mikakati ya
kuhifadhi misitu ambayo takwimu zinaonesha zaidi ya hekta laki nne zinapotea
kila mwaka kutokana na ukataji wa miti.
“Kutokana
na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti tuna kazi kubwa ya
kufanya, kwanza lazima tuhame twende katika nishati safi ya kupikia na *kwa*
uzinduzi wa mkakati wa nishati safi ya kupikia tuna afua mbalimbali
zinatekelezwa kuhakikisha kwamba suala la uharibifu wa mazingira,” amesema.
Aidha,
Dkt. Jafo amesema kuwa pamoja na mikakati hiyo pia Serikali kupitia Ofisi ya
Makamu wa Rais inaendelea kusimamia utekelezaji wa zoezi la upandaji wa miti
katika kila Halmashauri ambapo imeelekezwa zipande miti milioni 1.5 kila mwaka.
Amewahimiza
wananchi na taasisi kupanda miti na kuitunza kwani katika lengo la Serikali la
kupanda miti milioni 266 kwa Halmashauri zote ni miti milioni 211 sawa na
asilimia 76.5 ndio imestawi.
Post a Comment