********** Na Mwandishi Wetu
Halmashauri na Serikali za Mitaa zimeaaswa kuongeza uelewa
kuhusu umuhimu wa teknolojia saidizi kupitia mikutano ya Kijiji, redio za
kijamii na vikao vya Halmashauri pamoja na kushirikisha jamii katika kupunguza
unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu ili kutoa fursa zinazostahili kwa wazee wenye
udhaifu na Walemavu badala ya kuwaficha.
Hayo yamebainishwa Leo Juni 4, 2024 jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi Ofisi ya Waziri Kuu, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Rasheed
Maftah wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kuadhimisha siku ya
kimataifa ya teknolojia saidizi Kwa mara ya kwanza nchini Tanzania.
Amesema kuwa uboreshaji wa teknolojia saidizi ni muhimu Kwa
kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) na kuhakikisha kuwa hakuna mtu
anayeachwa nyuma, ikiwa ni haki muhimu ya binadamu katika kupunguza Umasikini
na kutengeneza usawa, hivyo Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na
kuridhia mikakati ya kimataifa kama vile Mkataba wa Mataifa wa Haki za Watu
wenye ulemavu, kuandaa sera za Kitaifa za ulemavu ya 2004 na Sera ya Afya ya
2007.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa HelpAge Tanzania ambao ni
wadau katika kuboresha maisha ya wazee nchini, Smart Daniel amesema wazee wamekuwa wakikabiliwa na
changamoto ya kukosa vifaa visaidizi, ambapo karibu asilimia 66 ya wazee wote
wanahiyaji aina mojawapo ya vifaa hivyo, na kwa watu wenye ulemavu karibu
Milioni 7.1 ya watanzania wote pia Wana mahitaji hayo, hivyo upo umuhimu wa
Taifa kuweka mikakati maalum wa upatikanaji wa vifaa visaidizi kwa wenye
uhitaji.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya watu wenye
ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Jonas Lubago ametoa wito Kwa Serikali kuongeza
jitihada mbalimbali ikiwemo kuwashawishi wazalishaji wa vifaa visaidizi wa
ndani ya nchi ili kupunguza gharama, kuongeza upatikanaji na kufanya vifaa
hivyo kuendana na mazingira husika ya Kitanzania.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watu wanaohitaji
Teknolojia Saidizi inaongezeka, huku kidunia ni zaidi ya watu bilioni 2.5,
Tanzania ikikadiriwa kuwa na watu Milioni 7.5 wenye uhitaji wa vifaa hivyo,
ambapo Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, inakadiriwa
kuwa Watu Milioni 3.4 sawa na asilimia
5.7 ya watanzania wote ni wazee, huku ikikadiriwa kuwa ifikapo 2050 idadi ya
wazee itafikia Milioni 10.
Post a Comment