**********
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewataka Watanzania kuzingatia utamaduni wao na katu wasiendekeze
utamaduni wa kigeni kwan kwa kufanya hivyo ni sawa na kuuza uhuru wao kama
nchi.
Dkt. Biteko amesema hayo Juni 27, 2024 katika viwanja vya
Kisesa, wilayani Magu, Mkoani Mwanza wakati akimwakilisha Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan kufunga tamasha la Utamaduni wa Kisukuma, Bulabo lililoshirikisha
watemi kutoka mikoa sita ya Kanda ya Ziwa na Mkoa wa Tabora.
“Utamaduni wetu unatupa heshima na tamasha kama hili
linatuwezesha kama nchi kuzingatia utamaduni wetu na kuwawezesha Watanzania
kujitambua, kitendo cha kuiga utamaduni wa nchi nyingine bila kupima madhara
unaweza kutuharibia na kuondoa heshima yetu”
Aliongeza kuwa “Vitendo vya mmomonyoko wa maadili
vinavyoendelea katika maeneo mbalimbali nchini havina mizizi katika utamaduni
wa Watanzania na jamii za kiafrika, hivi sasa tunashuhudia vitendo kama mauaji
ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino),
Mapenzi ya jinsia moja na Unyanyasaji wa kijinsia ni baadhi ya mambo
yanayotokana na vitendo vya kuiga kutoka maeneo mengine”.
Aidha, Dkt. Biteko amesema utambuzi wa makabila miongoni mwa
Watanzania ni kwa ajili ya kutaniana na sio kwa ajili ya kubaguana miongoni
mwao kutokana na Utamaduni wa Watanzania kuishi kama familia moja na hivyo
amehimiza kufanyika kwa matamasha mengi ya utamaduni ili kuenzi mila na
kudumisha utamaduni wa Mtanzania.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewataka Watanzania
kujipanga vema kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa
pamoja na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2025, “Chagueni viongozi wenye
uwezo wa kuwaongoza na kuwaletea maendeleo hata kama hawana fedha na katu
msiingie kwenye mtego wa kuchagua viongozi wasio na uwezo kwa kigezo cha fedha”
alilisitiza Dkt. Biteko.
Awali, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt.
Damas Ndumbaro amesema Serikali kupitia wizara kwa kushirikiana na watemi wa
maeneo mbalimbali imepanga kufanya tamasha kubwa zaidi litakalofanyika katika
Viwanja vya Majimaji, Songea Mkoani Ruvuma.
Naye, Kiongozi wa Umoja wa Watemi nchini Anthoni,
Ameishukuru Serikali kwa kuwatambua na kuwawekea mazingira rafiki katika
kuendeleza matamasha ambayo yanaendeleza mila na desturi kutoka maeneo
mbalimbali ya nchi yetu, Tamasha la Utamaduni wa Wasukuma limeshirikisha watemi
kutoka mikoa saba ambayo ni Mwanza, Kagera, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na
Tabora.
Mwisho.
Post a Comment