Na Abdallah Nassoro-WHITE SAND
Wizara ya Afya imeeleza umuhimu wa kuwa na chombo huru kitakachokuwa na jukumu la kutoa ithibati na kudhibiti ubora wa huduma za Afya zinazotolewa nchini ili kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na kukuza utalii tiba nchini.
Hayo yamesemwa leo Juni, 18, 2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe aliyemwakilisha Waziri wa Afya wakati wa ufunguzi wa kongamano la siku moja la wataalam wa afya wa Tanzania na Uingereza linaloendela katika hoteli ya White Sands, jijini Dar es Salaam.
“Nawapongeza sana taasisi ya TUHEDE ambao ni watanzania wanaoishi nchini Uingereza (Diaspora) ambao wanashirikiana na na Taasisi zetu za Afya hapa nchini katika mafunzo, tafiti na ubunifu ikiwemo matumizi ya TEHAMA katika tiba, swala ambalo litapelekea huduma zetu za ubingwa na ubingwa bobezi kuboreka na hivyo kuwezesha nchi yetu kuwa kitovu cha tiba utalii kwa nchi zinazotuzunguka"
"Niwaombe sana wataalamu hawa pamoja na maeneo hayo ambayo tumeanza kushirikiana, tushirikiane nao pia katika kuandaa miongozo na hatimae chombo ambacho kitakuwa na jukumu la kutoa ithibati ya utoaji wa huduma za afya kwa lengo la kudhibiti ubora wa huduma za afya nchini kama wanavyofanya nchini Uingereza. Nimesikiliza mada ya mtaalamu kutoka Uingereza ambae ameeleza namna mfumo wa ithibati na udhibiti ubora wa huduma za tiba unavyofanyika na namna wanavyochukua hatua stahiki nikaona na sisi tunaweza kufanya hivyo".
Amesema tayari zipo taasisi na mabaraza ambayo yanafanya kazi hiyo lakini bado kuna maboresho yanayotakiwa kufanyika kwa lengo la kujiweka katika nafasi ya juu zaidi kwa.kufuata vigezo vya kitaifa na kimataifa.
Ameongeza kuwa “Tunahitaji kuwa na chombo huru kitakachotuambia hapa tunafanya vizuri na hapa hatufanyi vizuri, kwa lengo la kuboresha huduma zetu zaidi na zaidi”
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma Prof. Abel Makubi amesema kongamano hilo la kitaaluma lina lengo la kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya matibabu.
Kwa upande wake Mwekahazina wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Uingereza wanaojihusisha na masulaaya afya (TUHEDA) Prof. Gideon Mlawa amesema ushirikiano baina jumuiya hiyo na Tanzania utajikita zaidi katika kubadilishana wataalam, mafunzo na tafiti kwa lengo la kuboresha huduma.
“Katika ushirikiano huu sisi Watanzania tunaoishi Uingereza tunarudisha nyumbani kile tulichokipata ikiwa ni pamoja na utaalam, lakini pia tutaenda kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kuinua sekta ya afya nchini” amesema
Wataalam wa Afya kutoka hospitali za Taifa, Rufaa Kanda na Mikoa wamekutana na wenzao kutoka Hospitali Queen-Elizabeth ya Uingereza chini ya uratibu wa TUHEDA ili kujadiliana mbinu mbalimbali za uboreshaji wa tiba na huduma za afya nchini
.jpeg)

.jpeg)


Post a Comment