MADIWANI WATAJA CHANZO CHA UTOROSHWAJI KAHAWA B'MULO

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Leo Rushahu,akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani
Mwonekano wa zao la kahawa

.............

Na Daniel Limbe,Biharamulo

BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera limesema chanzo kikuu cha wakulima kutorosha na kuuza kahawa yao kwa magendo ni kutokana na vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) kukosa fedha taslimu za kuwalipa wakulima,hali inayoikosesha mapato halmashauri hiyo.

Aidha hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya wakulima kuwauzia walanguzi binafsi kahawa changa iliyopo mashambani ( Butula) kwa bei ya kinyonyaji kinyume cha sheria, licha ya mkuu wa mkoa huo, Fatma Mwasa,kutangaza bei elekezi ya shilingi 3700 kwa kila kilo katika msimu wa kilimo wa 2024/25.

Kutokana na hali hiyo wameiomba serikali pamoja na taasisi za kifedha kuzikopesha Amcos hizo ili ziweze kujiendesha hatua itakayosaidia kuinua mapato ya kaya,wilaya na taifa kwa ujumla.

Diwani wa kata ya Kalenge,Erick Method, pamoja na diwani wa kata ya Kabindi,Philibert Rubula, wamedai kuwa ongezeko la wanunuzi wa kahawa changa(Butula) linatokana na wakulima wengi kukosa fedha za kukidhi mahitaji yao ya msingi jambo linalosababisha kuchukua fedha kwa wanunuzi wa magendo kabla ya kuanza mavuno ya kahawa.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu, ametumia fursa hiyo kuwaonya wanunuzi wa kahawa changa mashambani na kutaka wachukuliwe hatua kali za sheria,huku akimwagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhuisha vizuizi vya barabarani ili kudhibiti utoroshwaji wa kahawa kwenda nchi jirani kinyume cha sheria

 

0/Post a Comment/Comments