**********
Serikali
imezitaka Mamlaka na Taasisi zake zote kuimarisha na kuwezesha
vitengo vyake vinavyosimamia utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki ili
viweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya
Usimamizi wa Mazingira Sura 191 na kanuni zake.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis
wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Asha Abdullah Juma aliyeuliza Serikali ina
mkakati gani wa kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki.
Akiendelea
kujibu swali hilo, Mhe. Khamis amesema kuwa Serikali imeweka mikakati
mbalimbali ya kuhakikisha mifuko ya plastiki ambayo ilipigwa marufuku
inadhibitiwa.
Ametaja
mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za matumizi ya
mifuko ya plastiki zikiwemo za kiafya na kimazingira endapo itazagaa.
Halikadhalika,
Naibu Waziri Khamis amesema Serikali ilipiga marufuku uzalishaji, matumizi
uingizaji, usambazaji na usafirishaji nje ya nchi mifuko ya plastiki nchini
kuanzia tarehe 01 Juni, 2019.
Pamoja
na mikakati hiyo, pia Serikali ilitunga Kanuni za Kupiga Marufuku Mifuko
ya Plastiki za Mwaka 2019 kupitia Tangazo la Serikali Na.394 la 2019 ili
kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki isiyofaa.
Hivyo,
Naibu Waziri Khamis ametoa wito kwa Asasi za Kiraia pamoja na wananchi kwa
ujumla kushirikiana na Serikali katika kupambana na matumizi ya mifuko ya
plastiki.
Akijibu
swali la nyongeza kuhusu mpango wa Serikali wa kuwabana wanaozalisha
vifungashio na mifuko isiyokidhi vigezo, Mhe. Khamis amesema sheria ipo na inafanya
kazi kwa kusimamiwa kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(NEMC).
“Nichukue
fursa hii kuwapongeza wenzetu wa NEMC wanafanya kazi kubwa ya utekelezaji wa
sheria hii na kama kuna haja ya kuifanyia marekebisho sheria hii tutafanya
hivyo,“ amesema.
Ameongeza
kuwa Serikali kupitia Baraza hilo imekuwa ikifanya doria katika viwanda kubaini
wanaokiuka sheria sanjari na kutoa elimu kwa wamiliki hao ili kuwajengea uelewa
kuhusu umuhimu wa kufuata sheria.
Pia, akijibu swali la Mbunge wa Pandani Mhe. Maryam Omar Said kuhusu Serikali kuhakikisha vifungashio na mifuko iliyoruhusiwa inapatikana kwa wingi, Naibu Waziri Khamis amesema kuwa Serikali inaendelea kuwahamasisha wawekezaji waendelea kuizalisha kwa wingi.
Post a Comment